2015-07-20 11:35:00

Jifunzeni kujipumzisha mkiwa na Yesu ili mpate kuhudumia vyema!


Ndugu wapendwa, jumapili hii twaweza kuiita jumapili ya huruma kwa kundi. Ni mwaliko wa wajibu wa kikristo. Ni mwito wa kuwa tayari kuhudumia kikristo. Masomo yetu ya leo yanatuonesha hali hiyo.

Katika somo la kwanza – tunasikia kuwa sababu ya viongozi wakatili, taifa la Mungu limepoteza dira. Ila mpango wa Mungu wa ukombozi ni tofauti kabisa na mpango wa mwanadamu. Hivyo Mungu anamtuma mjumbe wake mwaminifu, Nabii Yeremia kutangaza kwamba Mungu hataacha mpango wake wa mapendo na kwamba anawaandalia watu viongozi wapya. Nabii Yeremia alibaki mwaminifu kwa Mungu kuliko kuwafuata viongozi wabadhilifu. Sisi twaitwa kondoo kwa vile Mungu ni mchungaji na hapa kondoo wanapata maelezo sahihi na hupata nafuu ya ulinzi na maongozi ya Mungu. Uaminifu, ulinzi na urafiki ni alama za mchungaji mwaminifu. Mpango huu ulikamilika kwa ujio wake Kristo.

Katika somo la pili, twaona kuwa uwepo wa Kristo, huondoa migawanyiko yote ya kibinadamu. Paulo anajiita mtumwa wa Kristo.

Katika Injili, twaona kuwa Yesu anataka kujitenga kidogo na watu ili apate muda wa kusali na kupumzika. Lakini watu wanamfuata. Jambo hili linamgusa sana. Kwa watu hawa wenye njaa na kiu ya ukweli, yeye anawapatia Neno la uzima. Yesu anaona kundi lenye njaa na kiu na anachukua uongozi wa hilo kundi na kuwafundisha tena kwa mpangilio na kutuliza njaa na kuwapa ulinzi kamili. Mchungaji mwema yuko makini na kufanya kazi yake kwa uaminifu.

Ndugu wapendwa, tunaona kuwa Mungu anajitoa kwa upendo na matokeo yake ni uzima. Na ikiwa watu wanajibu, matokeo yake ni wokovu na uzima pia. Wale wanaoguswa na upendo huu, hutangaza huo wokovu. Ndicho alichofanya Yesu, alipowaaminisha utume na akawatuma ulimwenguni kwenda kuhubiri habari njema.

Katika Injili ya Marko ni mahali pekee hapa wale 12 wanaitwa mitume, yaani waliotumwa. Pengine pote wanaitwa wafuasi, yaani wanafunzi. Hivyo yule aliyetumwa anakuwa sehemu ya wokovu wa watu kwa kutangaza hiyo habari njema. Huu ndio wajibu wetu leo. Kuwa wachungaji wema kama alivyokuwa Kristo, mchungaji mwema. Hii itawezekana tu kama tutakaa pamoja na Kristo na kujazwa na roho wake.

Nabii Yeremia anatupa changamoto kubwa leo tunaposikia tena Neno la Mungu na kutafakari nafasi yetu katika kutangaza hiyo habari njema. Nabii Yeremia hakutishwa na viongozi dhalimu, ila alimtumainia Mungu na akakemea waziwazi maovu ya viongozi wabovu.

Bwana wetu Yesu Kristo anatupa changamoto kubwa zaidi leo kama wafuasi wake. Anatoka katika hali yake ya ubinafsi na kuwahurumia wahitaji. Tunapoangalia hali zetu, nchi yetu, ulimwengu wetu wa leo na hali zetu na mitindo yetu ya maisha tunajiuliza je tunatakiwa kufanya nini? Hatuna budi kujiuliza ni kipi kilio cha watu wetu leo? Ni kitu gani hasa tunahitaji? Kidini, kisiasa, kiuchumi, kimaadili n.k?

Ni mambo gani ambayo tunatakiwa tuyape kipaumbele ili huruma ya Kristo ionekane wazi? Je, tunajitenga na wenye shida na mahitaji zaidi yetu na kusema shauri yao? Yesu hakufanya hivyo. Watumishi waaminifu wa Mungu hubaki upande wa Mungu hata pale wanapojikuta katika mazingira magumu ya kutoa ushuhuda. Upendo kwa Mungu na moyo wa ushuhuda huwafanya wajisahau katika mahitaji yao binafsi kama kupumzika na kujitoa kwa ajili ya wengine.

Inaonekana wazi kuwa Yesu alichoka na anaona wafuasi wake wamechoka. Wanataka kujitenga ili wapumzike. Lakini mahitaji au njaa na kiu ya watu inakuwa kubwa na Yesu anawahurumia. Anawalisha Neno la uzima. Na anachofanya kinatuliza njaa yao. Wanapata wokovu na uzima. Yesu hatoi ziada bali anajitoa mwenyewe na anawataka wafuasi wake wafanye hivyo hivyo. Nasi tukafanye hivyo.

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.