2015-07-13 09:20:00

Mwilisheni imani katika mshikamano wa upendo na huduma!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili asubuhi tarehe 12 Julai 2015 ametembelea Eneo la Bando Norte, kitongoji ambacho ni maskini sana nchini Paraguay na kwamba, Kanisa kwa kushirikiana na Serikali limeanzisha miradi kadhaa katika eneo hili kwa lengo la kuboresha maisha ya watu. Baba Mtakatifu amesikiliza kwa umakini mkubwa shuhuda mbali mbali zilizotolewa na wananchi katika eneo hili jinsi wanavyopambana na maisha, ili kulinda utu na heshima yao; kuwa na makazi bora ili kujikinga na mvua za mara kwa mara ambazo hivi karibuni zimesababisha mafuriko makubwa.

Baba Mtakatifu amekumbushia historia ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; iliyolazimika kukimbilia Misri ili kutafuta hifadhi ya Mtoto Yesu. Huku kulikuwa ugenini na hakuna hata mtu waliyekuwa wanafahamiana naye; hawakuwa na nyumba wala ndugu. Maria na Yosefu walibahatika kupata Mtoto wao Yesu; familia ya watu watatu, pweke katika nchi ya ugenini. Ni Familia iliyotegemea kupata mahitaji yake kutokana na huruma kwa watu waliokuwa wanawazunguka.

Wachungaji waliokuwa kondeni waliposikia Habri Njema ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu walijitokeza na kuonesha upendo na mshikamano kama majirani wema; wakawa ni sehemu ya Familia ya Yesu, Maria na Yosefu. Hivi ndivyo inavyotokea Yesu anapoamua kuingia katika maisha ya waamini na haya ni matunda ya imani inayowawezesha watu waliokuwa mbali kuwa majirani. Imani inawahamasisha watu kujenga umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Uwepo wa Yesu katika maisha ya waamini unawaamsha na kuwategemeza.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, imani isiyomwilishwa katika mshikamano wa upendo, ni imani ambayo imekufa kwani haina mvuto wala mashiko. Hii ni imani ambayo haimwambati Yesu, Mwenyezi Mungu wala jirani. Mwenyezi Mungu ndiye aliyeonesha mshikamano wa kwanza na binadamu kwa kufanyika Mwili na kukaa kati ya ndugu zake. Imani inayomwambata Yesu inawawezesha waamini kuwa na ndoto ya leo na kesho iliyo bora zaidi pamoja na kuthubutu kupambana kila siku, ili kupata maisha bora zaidi.

Nia ya Baba Mtakatifu Francisko kutembelea eneo la Banado Norte ni kuwatia ari, nguvu na shime waamini na wananchi wa sehemu hii kuwa Wamissionari; kwa kumwilisha imani yao katika matendo katika medani mbali mbali mbali za maisha. Ni mwaliko na changamoto ya kuwa jirani na vijana pamoja na wazee; wawe ni nguzo na matumaini kwa familia changa; kwa wale wote wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha; ili waweze kuwasindikiza, kuwasaidia na kuendelea kuhamasisha tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.