2015-07-11 14:33:00

Msikubali kuyumbishwa katika misingi ya maadili na utu wema!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, limesikitishwa na mwelekeo unaoendelea kuoneshwa na nchi za Ulaya na Marekani kwa kushabikia na hatimaye kupitisha sheria zinazoruhusu ndoa za watu wa jinsia moja, kama ilivyojitokeza kwenye kura ya maoni iliyofanyika nchini Ireland na uamuzi wa Mahakama kuu ya Marekani kuruhusu ndoa za jinsia moja kwa nchi nzima. Maaskofu wanasema, hizi ni dalili za watu kukengeuka na kutopea katika dhambi, kwa kisingizio cha uhuru wa mtu binafsi.

Taarifa zinaonesha kwamba, ndoa za watu wa jinsia moja ni jambo la kawaida nchini Ireland, Canada, Hispania, Ufaransa na Marekani. Kuna baadhi ya wanasiasa Barani Ulaya wanaoendelea kutoa shinikizo kwa nchi ambazo hazina sheria hii, kuhakikisha kwamba, zinatunga sheria hiyo haraka iwezekanavyo. Kutokana na mwelekeo huu, athari zake zinaweza kuwa kubwa hata kwa vijana wa Nigeria, kwani nchi ambazo zimepitisha sheria hii ni zile nchi ambazo kimsingi pia zina uwezo mkubwa katika njia za mawasiliano ya jamii.

Hapa vijana wanatakiwa kuwa makini, vinginevyo wanaweza kujikuta wakimezwa na malimwengu na kuwa kama kichwa cha mwendawazimu. Njia za mawasiliano ya jamii zina umuhimu sana katika ustawi na maendeleo ya binadamu, lakini zisipotumiwa vyema zinaweza kuwa ni chanco kikuu cha majanga, hali ya watu kukengeuka na kutopea katika dhambi. Kukubali ndoa za watu wa jinsia moja, ni kuhatarisha tunu msingi za maisha ya familia na hapa ni mwanzo wa kukumbatia utamaduni wa kifo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linawaalika wanasiasa, watunga sera na wananchi wa Nigeria katika ujumla wao kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika masuala ya ndoa za watu wa jinsia moja kwa kisingizio cha uhuru na haki msingi za binadamu. Wanahabari wasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kukazia kanuni maadili na utu wema. Kamwe vyombo vya mawasiliano ya jamii visikubali kuwa ni wakala wa mmong’onyoko wa maadili kutoka Ulaya na Marekani. Wananchi wasimame kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na famili, utu na heshima ya binadamu; kanuni maadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.