2015-07-11 13:44:00

Mh. Padre George Bugeja ateuliwa kuwa Askofu mwandamizi Tripoli, Libya!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre George Bugeja, O.F.M, msimamizi wa nyumba ya kitawa ya Mtakatifu Anthoni wa Padua, Gozo, Malta, kuwa Askofu mwandamizi wa Vikarieti ya Tripoli, Libya. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule George Bugeja alikuwa ni afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Askofu mteule George Bugeja alizaliwa tarehe Mosi Julai 1962 huko Xaghara, Jimbo Katoliki la Gozo, nchini Malta. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 28 Agosti 1983 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 5 Julai 1986 akapadrishwa.

Tangu wakati huo ameendelea kutekeleza dhamana na utume wake wa kichungaji Jimbo Katoliki la Gozo kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 2004. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mama yetu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu huko Sliema. Kunako mwaka 2008 hadi mwaka 2010 alikuwa ni Mzee wa Baraza katika Mahakama ya Kanisa.

Kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015 alikuwa anafanya utume wake kama Afisa mwandamizi kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Kuanzia mwezi Marchi 2015 aliteuliwa kuwa ni msimamizi wa nyumba ya kitawa ya Mtakatifu Anthony wa Padua huko Ghajnsielem, Gozo.

Itakumbukwa kwamba, Vikarieti ya kitume ya Tripoli, Libya ilianzishwa kunako mwaka 1937 ina jumla ya wakazi 6, 204, 000 na kati yao Waamini wa Kanisa Katoliki ni 50, 000. Waamini wote hawa kwa sasa wanahudumiwa kwenye Parokia moja, huduma inayotolewa na Padre mmoja wa Jimbo akisaidiana na watawa watatu wa kiume na watawa 8 wa kike. Vikarieti hii imekuwa ikuhudumiwa na Askofu Giovanni Martinelli, mwenye umri wa miaka 73 na ambaye kwa sasa afya yake ina chechemea sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.