2015-07-10 15:27:00

Francisko ni Papa wa maskini na mjumbe wa imani, matumaini na mapendo!


Rais Evo Morales wa Bolivia katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini mwake, amemshukuru kwa namna ya pekee kuja kuwaona na kuwafariji, ili hatimaye, kuwapatia ujumbe wa matumaini katika hija ya maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu ndani ya moyo wake anasema Rais Morales anabeba ujumbe wa imani, matumaini na ukombozi.

Haya ni maneno ambayo Rais Morales ameyasema kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa El Alto, wakati umati mkubwa wa wananchi wa Bolivia ulipofurika ili kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini humo, kuanzia tarehe 8 Julai 2015. Wananchi wa Bolivia wamemkubali na kumpokea kwa mikono miwili kama “Papa wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii”.

Kwa mwamini yeyote anayemsaliti maskini, atambue kwamba, anamsaliti Yesu Kristo aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote waliokuwa wantengwa na jamii. Kumbe, anayemsaliti maskini, anamasaliti Khalifa wa Mtakatifu Petro na hatimaye anamsaliti Yesu Kristo mwenyewe. Kwa namna ya pekee, Rais Morales anasema, Baba Mtakatifu Francisko anafanana na Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kuambata ufukara, nguzo muhimu sana katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko miongoni mwa Wakristo, ili mali dunia iweze kutumika kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia maskini katika maisha yao kiroho na kimwili.

Rais Morales anakaza kusema, wananchi wa Bolivia wanaupokea ujio wa Baba Mtakatifu kwa imani na matumaini makubwa na kwamba, wanaonja uwepo wake wa karibu, unaotoa matumaini yanayookoa na kumkomboa mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.