2015-07-06 10:00:00

Dolla millioni 2. 1 kutumika kama ruzuku ya maendeleo kwa Kanisa Barani Afrika


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limechangia zaidi ya millioni moja nukta mbili za Kimarekani kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Uamuzi huu umetolewa hivi karibuni baada ya Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kwa ajili ya Kanisa Barani Afrika kumaliza kikao chake kilichokuwa kinafanyika huko St. Louis, Marekani.

Fedha hii italiwezesha Kanisa Barani Afrika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, ili waweze kupambana na umaskini. Fedha inapania pia kutoa majiundo endelevu kwa Makatekista ni mihimili ya Uinjilishaji Barani Afrika pamoja na kuimarisha utume wa familia na imani katika ujumla wake.

Akizungumzia kuhusu ruzuku hii kwa ajili ya Kanisa Barani Afrika, Kardinali Theodor McCarrick, Rais wa Tume anasema, Familia ya Mungu Barani Afrika limekuwa ikitumia vyema fedha ya ruzuku inayotolewa kwa ajili ya kusaidia majiundo makini kwa mihimili ya Uinjilishaji sanjari na kuwaandaa viongoni walei, watakaosaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Angola ni kati ya nchi za Kiafrika zitakazofaidika na ruzuku hii kutoka Marekani, ili kusaidia juhudi za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; kwa kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa vitendo vya kibaguzi dhidi ya wahamiaji vilivyofanywa hivi karibuni Afrika ya Kusini. Msaada kwa Kanisa Katoliki nchini Ethiopia unapania kusaidia juhudi za kuendeleza utume wa familia, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa familia.

Liberia itapata msaada ili kuiwezesha kuwajengea uwezo Wanawake Wakatoliki ili kuweza kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia utu na heshima ya binadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linabainisha kwamba, fedha hii ni kielelezo cha ukarimu na mshikamano wa udugu unaooneshwa na Familia ya Mungu kutoka Marekani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika. Lengo ni kulisaidia Kanisa kujenga uwezo wa kujitegemea katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.