2015-07-02 15:38:00

Hayati Patriaki Nerses Bedros alikuwa ni kiongozi aliyeguswa na shida za watu


Patriaki Nerses Bedros wa XIX Tarmouni wa Kanisa la Cilicia ya Warmeni, aliyefariki dunia hapo tarehe 25 Juni 2015 amezikwa kwa heshima zote hapo tarehe 30 Juni 2015 na ibada ya mazishi kuhudhuriwa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki. Katika Ibada hii, Kardinali Sandri amewasilisha salam za rambi rambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anakaza kusema, ni kiongozi aliyekuwa msikivu kwa mateso na mahangaiko ya wananchi wa Armenia.

Marehemu Patriaki Nerses Bedros aliyakita maisha yake katika mwamba thabiti ambao ni Yesu Kristo mwenyewe. Kama Askofu alitambua na kuthamini huduma aliyokuwa amekabidhiwa kwa ajili ya Kanisa la Kristo, yaani kulinda, kutunza na kudumisha imani. Akataka kuona imani hii inamwilishwa katika matendo ya kila siku, ndiyo maana katika maisha na utume wake, akatoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya majiundo makini ya Wakleri, ili hata katika shida na mahangaiko, wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa waweze kusimama imara ili kumshuhudia Kristo na Kanisa lake, wakitambua kwamba, Kristo ni chemchemi ya matumaini na faraja kwa binadamu.

Ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Elia, mjini Beiruti, imehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya  Lebanon. Baba Mtakatifu Francisko bado anakumbuka jinsi walivyoshirikiana kwa karibu katika maadhimisho ya miaka mia moja ya mauaji ya kimbari dhdi ya Warmeni sanjari na kumtangaza Mtakatifu Gregorio wa Narek kuwa Mwalimu wa Kanisa, katika Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, hapo tarehe 12 Aprili 2015.

Kwa Hayati Patriaki Nerses Bedros, kumbu kumbu ya maadhimisho ya miaka mia moja ya mauaji ya kimbari dhidi ya Warmeni, lilikuwa ni tukio ambalo lilipaswa kukumbukwa kwa haki, ili kuangalia mateso, dhuluma na nyanyaso walizokumbana nazo Wamerni, lakini kwa neema na huruma ya Mungu, wakasimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Hili ni tukio ambalo linapaswa kuwa ni faraja na mwanzo wa mchakato wa upatanisho wa kitaifa; ili kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ya kuganga na kuponya madonda yanayoendelea kuwatesa wengi hadi nyakati hizi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuiga mfano wa maisha na utume wa Patriaki Nerses Bedros na kwamba, tasaufi ya Mtakatifu Gregori wa Narek, Mwalimu wa Kanisa, iwe ni mfano kwa viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao. Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu ili aendelee kulipyaisha Kanisa kwa nguvu zake, kwa kumtolea mateso na mahangaiko ya Familia ya Mungu inayoendelea kufanya hija ya maisha ya kiroho hapa duniani. Amewatakia wote walioshiriki katika Ibada hii, baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.