2015-07-01 11:47:00

Iweni ni vyombo vya upatanisho, haki na amani!


Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, tarehe Mosi Julai 2015 wanaadhimisha rasmi kilele cha Jubilei ya Miaka 200 tangu Mtakatifu Gaspar del Bufalo alipoanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kunako tarehe 15 Agosti 1815. Tukio hili la kihistoria, limetanguliwa na maandalizi yaliyofanywa kwenye nyumba na Parokia za Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu na hatimaye, kufanya hija ya pamoja mjini Roma.

Lengo ni kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa miaka 200 ya uwepo wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, tayari kujibu kilio cha damu kwa watu wa nyakati hizi, kwa kutambua kwamba, wao wanapaswa kuwa kweli ni vyombo vya upatanisho, haki na amani, hasa katika ulimwengu mamboleo ambamo unasheheni kinzani, misigano na mipasuko ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kidini.

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania wamefika mjini Roma wakiwa wameambatana na kundi kubwa la mahujaji kutoka Parokia mbali mbali zinazohudumiwa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania. Mahujaji hawa wanatembelea maeneo ya kihistoria kwa maisha ya Kanisa la Kiulimwengu, lakini kwa namna ya pekee kuhusiana na maisha na utume wa Mtakatifu Gaspar, mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu, mto wa rehema na chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu.

Wamissionari pamoja na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumanne jioni, tarehe 30 Juni 2015, wameshiriki katika Ibada ya Upatanisho kwenye Parokia ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, iliyoko Jimbo kuu la Roma kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya toba na upatanisho, tayari kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, tarehe Mosi, Julai 2015. Katika Ibada hii, Familia ya Mtakatifu Gaspar, imesikikiliza shuhuda zilizotolewa kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kukazia umuhimu wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, ili kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho katika ukweli na uwazi.

Kwa upande wake, Padre Joseph Nasal, kutoka Marekani amekaza kusema, upatanisho ni mahali ambapo, haki, ukweli, huruma na amani vinakumbatiana na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Kuna haja kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga maeneo ambayo ni wazi na salama katika historia na maisha ya watu; ili kuwapokea na kuwakaribisha wengine, tayari kujenga utamaduni wa kusikiliza magumu, changamoto na furaha zinazofunuliwa na jirani zao katika hija ya maisha yao.

Padre Joseph Nasal anakaza kusema upatanisho unapania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha mahusiano kati ya watu na kati ya mtu na nafsi yake. Damu Azizi ya Yesu, inawachangamotisha Wamissionari kuwa kweli ni wahudumu wa uponyaji, amani na upendo.  

Kwa uapnde wake, Padre Juan Carlos Barajas, Kutoka Amerika ya Kusini anasema kwamba, madonada ya kinzani, chuki na utengano yanaathari zake kwa watu mbali mbali, lakini yanaacha chapa ya kudumu kwa mhusika mwenyewe. Kumbe, hapa kuna haja ya kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya toba na msamaha wa kweli unaoponya madonda kutoka katika undani wa mtu. Ikumbukwe kwamba, mchakato wa upatanisho unalenga kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, ili kujenga, kudumisha na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mchakato wa upatanisho hauna budi kuanza katika undani wa mtu binafsi na matunda yake, kuonekana kwa wengine.

Padre Terenzio Pastore, kutoka Italia katika ushuhuda wake, amefanya rejea kwa ushuhuda uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Papa Yohane Paulo II anasema, hakuna amani pasi na haki na wala hakuna haki pasipo na msamaha; haya mambo yote yanategemeana na kukamilisha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema kwamba, amani ya kweli ni matunda ya haki inayopaswa kujikita katika msamaha wa kweli unaoganga na kutibu madonda makubwa katika maisha ya mwanadamu. Ili kufikia haki ya kweli kuna haja ya kujikita katika msamaha kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kumtembelea Ali Agca, aliyefanya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Bila msamaha wa kweli, dunia itageuka kuwa ni uwanja wa fujo anasema Padre Terenzio Pastore.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.