2015-06-30 15:03:00

Papa Mstaafu Benedikto XVI yuko mapumzikoni Castel Gandolfo


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 30 Juni 2015 amekwenda kumtembelea, kumsalimia na kumuaga Papa mstaafu Benedikto XVI anayeondoka kwenda Castel Gandolfo, kwa muda wa majuma mawili kama sehemu ya mapumziko ya kipindi cha kiangazi, wakati huu watu wengi wanapoukimbia mji wa Roma, ili kutafuta hifadhi ya kipindi cha joto. Papa mstaafu Benedikto XVI anatarajiwa kurejea tena mjini Vatican tarehe 14 Julai 2015. Mazungumzo kati ya viongozi hawa wa Kanisa yamedumu kwa takribani nusu saa.

Wakati huo huo, Katekesi za Baba Mtakatifu Francisko zinazotolewa kila siku ya Jumatano zimefutwa kwa mwezi wote wa Julai. Baba Mtakatifu ataanza tena katekesi zake, mwanzoni mwa Mwezi Agosti, na zitakuwa zinafanyika kwenye Ukumbi wa Paulo VI. Baba Mtakatifu atakutana na Chama cha Uamsho wa Roho Mtakatifu, Jumatano jioni. Baba Mtakatifu ataendelea kusali na kutafakari na waamini kila Jumapili, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana.

Taarifa inaendelea kukaza kwamba, Ibada za Misa takatifu na waamini walei kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, kuanzia sasa zimesitishwa katika kipindi chote cha mwezi Julai na Agosti. Baba Mtakatifu Francisko ataanza kusali tena na waamini wakati wa Ibada ya Misa takatifu mwanzoni mwa Mwezi Septemba, 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.