2015-06-28 08:43:00

Wakristo wana dhamana ya kuimarisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo: Kanisa


Mitume Petro na Paulo ni miamba wa imani ya Kanisa: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, maadhimisho ya Sherehe ya Mitume hawa kwa uwepo wa wajumbe kutoka katika Kanisa Kiorthodox ni kielelezo makini cha upendo, ili neema ya Mungu iweze tena kuwaunganisha ili siku moja waweze kuwa wamoja katika imani, kama ilivyo katika Injili, Mababa wa Kanisa na hatimaye, waweze kushiriki Kikombe kimoja cha maisha ya kiroho.

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwenda kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, inayoadhimishwa na Mama Kanisa, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, kwa uwepo wa ujumbe kutoka katika Kanisa la Kiorthodox. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakumbuka kwa namna ya pekee kabisa, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Mtume Andrea, tukio ambalo limeacha kumbu kumbu ya furaha ya kudumu mioyoni mwao.

Ni matumaini ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwamba, ataweza kupata tena fursa mapema iwezekanavyo ya kuweza kufurahia umoja huu kati yao. Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, licha ya kashfa ya mpasuko unaoendelea kujionesha miongoni mwa Wakristo. Wakristo wanahamasishwa kujenga umoja kamili unaoonekana kwa kujikita katika msingi wa watakatifu, Petro na Paulo, miamba wa imani.

Ni kwa njia ya mahubiri na sadaka ya maisha yao, kiasi hata cha kumwaga damu yao, Injili ya Kristo imeweza kuenea sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, maadhimisho haya yawe ni fursa ya kujenga na kuimarisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; katika Mwili na Damu Azizi ya Yesu, kiini cha imani ya Kanisa. Kuna maendeleo makubwa yaliyokwishafikiwa na Makanisa haya mawili katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kupata suluhu ya kinzani na changamoto za kitaalimungu zilizoibuka ndani ya Makanisa kwa karne nyingi.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, Makanisa yanapaswa kuenzi mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa njia ya ushiriki mkamilifu; kwa kuwashirikisha wanataalimungu makini kutoka kwenye Makanisa haya ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, nje kabisa na mafao ya kisiasa hususan kuhusiana na “Nafasi na dhamana ya Kiongozi mkuu wa Kanisa”.  Makanisa haya mawili yanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, yanatangaza na kuwaonjesha watu Injili ya Furaha, matumaini na mapendo.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anachukua nafasi hii kumpongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuandika Waraka wake wa kichungaji kuhusu utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Anakumbusha kwamba, Kanisa la Kiorthodox, limekuwa mstari wa mbele katika harakati za kulinda na kutunza mazingira ambayo yanaendelea kuharibiwa kutokana matumizi ya binadamu, kama alivyobainisha kwenye Waraka wa kichungaji uliochapishwa kunako mwaka 1989 na Patriaki Demetrios pamoja na hotuba mbali mbali ambazo ameendelea kuzitoa ili kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira.

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Makanisa haya ni kujenga na kudumisha umoja kamili, kwa kuendeleza umoja unaojikita katika msingi wa Mitume, ili kuonesha kwamba, juhudi zao hazijapotea bure, ili imani ya Kanisa iweze kuenea sehemu mbali mbali za dunia. Salam na matashi mema kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza zimewasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza uliokuwa unaoongozwa na Askofu mkuu Giovanni kutoka Pergamo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.