2015-06-28 15:46:00

Imani kwa Yesu Kristo Mfufuka inaponya na kuokoa!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 28 Juni 2015, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro anasema kwamba, Yairo aliyekuwa mkuu wa Sinagogi alimwendea na kumpigia magoti Yesu, akimwomba aende nyumbani kwake, ili aweze kumponya binti yake alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili, ambaye alikuwa anatishiwa kifo. Sala hii ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya wazazi juu ya maisha, ustawi na maendeleo ya watoto wao.

Yairo anaonesha imani na matumaini kwa Yesu, hata baada ya kuambiwa kama mtoto wake alikwisha kata roho, bado aliendelea kumwamini Yes una kweli walipofika nyumbani kwake, Yesu akamwambia yule kijana, “Talitha kum” maana yake “Simama”. Kweli kijana akasimama na kuanza kutembea, matendo makuu ya Mungu. Hapa, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Yesu anaonesha nguvu yake dhidi ya kifo, ambacho anakifananisha na usingizi mzito ambao mtu anaweza kuamka na kuendelea na maisha yake kama kawa!

Mwinjili Marko katika mazingira ya tukio hili, anaongeza tena tukio jingine la mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, jambo ambalo kadiri ya tamaduni na mapokeo ya nyakati zile, lilimfanya kuwa najisi, kumbe asingeweza kukutana wala kukabiliana na watu wengine. Tayari alikwisha hukumiwa kifo cha kiraia.

Lakini, mwanamke huyu alionesha ushupavu wa pekee, akamfuata Yesu kati ya watu, kiasi cha kufanikiwa kugusa vazi la Yesu, aliyeshtuka, analipomwangalia yule mwanamke, akampatia maneno ya faraja! Mwanamke imani yako imekuponya! Hii ni sauti ya Mwenyezi Mungu inayomhakikishia mwanamke huyu kwamba, kamwe hajatengwa, na kwamba anaendelea bado kuwa ni mtoto wake licha ya ugonjwa unaomwandama.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, matukio yote haya yanafumbatwa katika imani inayoonesha kwamba, Yesu Kristo anaweza kuwaponya na kuwafufua kutoka katika mauti. Sehemu hii ya Injili inakazia kwa namna ya pekee imani kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, kielelezo cha ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti. Hii ndiyo imani ambayo Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliiungama na kuthibitishwa kwa namna ya pekee na Neno la Mungu katika Jumapili ya kumi na tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Yesu ana nguvu na uwezo juu ya mateso na kifo; anataka kuwapeleka waja wake wote nyumbani kwa Baba yake wa mbinguni ambako Injili ya maisha inatawala.

Ufufuko wa Yesu unaendelea kujionesha katika historia ya ulimwengu kama nguvu inayoleta upya wa maisha na matumaini kwa wale waliochoka na kukata tamaa ya maisha, wanachangamotishwa kujidhaminisha kwa Yesu, ili kuanza tena upya hija ya maisha yao. Imani ni nguvu thabiti na utimilifu wa maisha; anayemwamini Yesu, anatambua kwamba, Yesu ana nguvu ya kuweza kuongoza maisha na kuwaonjesha watu, hususan wanyonge, upendo wa Mungu unaookoa na kuponya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria awaombee zawadi ya imani thabiti na ujasiri, ili kuwa na matumaini na maisha kati ya ndugu zao.

Mara baada ya tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa umati mkubwa wa wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofanya maandamano ya amani, kuunga mkono dhana ya dunia kwa ajili ya familia ya binadamu. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kushirikiana kwa dhati katika kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya binadamu wote.

Anawapongeza wajumbe wa FOCSIV, Our Voices pamoja na wote walioshiriki katika maandamano haya. Anawatakia watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kupembua waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira, ”Laudato si” ”Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.