2015-06-27 16:02:00

Papa aunda Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican na kuteuwa viongozi wapya!


Baba Mtakatifu Francisko kwa utashi wake binafsi ameamua kuanzisha Sekretarieti ya mawasiliano itakayokuwa na wajibu pamoja na dhamana ya kuratibu shughuli zote za mawasiliano zinazofanywa na Vatican, ili hatimaye, kuwa na mfumo mmoja wa habari. Tangu wakati huu, vitengo mbali mbali vya mawasiliano vilivyokuwa vinajitegemea vitakuwa chini ya Sekretarieti ya mawasiliano ya Vatican, ili kuendeleza wajibu wa Kanisa katika uwanja wa mawasiliano ya jamii.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, taarifa ya Tume ya mawasiliano iliyoundwa hapo tarehe 30 Aprili 2015 ilishauri kwamba, Baraza la Kipapa la mawasiliano ya kijamii, Ofisi ya habari ya Vatican, Kitengo cha huduma za mitandao ya mawasiliano, Radio Vatican, Kituo cha Televisheni cha Vatican, Gazeti la L’Osserrvatore Romano, Kiwanda cha Uchapishaji Vatican, Huduma ya Picha na Duka la Vitabu la Vatican; zitakuwa chini ya Sekretarieti ya Mawasiliano ya Kijamii.

Kuanzia sasa, vitengo vyote hivi vitaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Sekretarieti ya mawasiliano na kwamba, Sekretarieti hii itatumia mtandao kwa anuani ifuatayo: www.vaticana.va. Hawa watakua na wajibu wa kuratibu ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa njia ya twitter inayotumia anuani ifuatayo: @pontifex.

Sekretarieti ya mawasiliano inaanza kutekeleza dhamana yake kuanzia tarehe 29 Juni 2015 na Makao makuu yake ya muda yatakuwa ni kwenye Jengo la Radio Vatican, yaani Piazza Pia, 3, 00120, Vatican.

Kutokana na mabadiliko haya, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Dario Edoardo Viganò kutoka Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV, kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti. Katibu mkuu atakuwa ni Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, mkuu wa kitengo cha mitandao ya kijamii cha Vatican. Mkurugenzi mkuu ni Dr. Paolo Nusiner, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la Avvenire, linalomilikuwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Mkurugenzi mkuu msaidizi ni Dr. Giacomo Ghisani, mkuu wa kitengo cha mahusiano ya kimataifa na sheria Radio Vatican. Pia ni mjumbe wa Baraza la uongozi wa Kituo cha Televisheni cha Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.