2015-06-27 17:06:00

"Ninakuja kwenu kama Msamaria mwema, ili kuwatangazia Injili ya Furaha"


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 13 Julai 2015 anatarajiwa kuwa na hija ya kitume huko Equador, Bolivia na Paraguay, nchi ambazo ziko Amerika ya Kusini. Kama sehemu ya maandalizi ya tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa huko Amerika ya Kusini, Baba Mtakatifu ameitumia Familia ya Mungu katika nchi hizi, ujumbe wa video, akionesha uwepo wake wa karibu, wema na shukrani. Anapenda kuwa kati yao, ili kushirikishana nao wasi wasi, matumaini na matarajio yao, ili kwa pamoja aweze kuwaimarisha katika imani na kufurahia pamoja nao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anataka kuwa ni shuhuda wa Injili ya Furaha, wema na ukarimu wa Mungu Baba yao wa mbinguni, hususan miongoni mwa watoto wake wanaohitaji zaidi. Hawa ni wazee, wagonjwa, wafungwa, maskini na wote wale ambao wameathirika kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.

Upendo wa Mwenyezi Mungu unaofumbata huruma, utawawezesha kugundua kwa namna ya pekee, uso wa Yesu Kristo, Mwanaye mpendwa, kaka na ndugu ya wote, kwani amejifanya jirani kwa ajili ya binadamu. Yesu mwenyewe amekiri na kusema kwamba, ni jirani kwa wote wanaoteseka na kusumbuka katika maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni Wasamaria wema kwa kutenda kama alivyotenda Yesu Kristo, kwa kuonesha ukaribu badala ya kufumba macho na kupita upande wa pili wa barabara au kuwageuzia kisogo wenye shida na mahangaiko: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuanzia sasa, anaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, akiwaombea wawe wadumifu katika imani, waoneshe ule moto wa mapendo na thabiti katika matumaini yasiyodanganya kamwe. Baba Mtakatifu anaitaka Familia ya Mungu katika nchi hiziĀ  tatu, kuunganisha sala zao na zake, ili Injili ya Kristo iweze kuwafikia wale wanaoishi pembezoni mwa jamii pamoja na kuendelea kusaidia tunu msingi za Ufalme wa Mungu ziweze kuyachachua malimwengu hata kwa nyakati hizi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anaiweka Familia ya Mungu huko Amerika ya Kusini, chini ya usimamizi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Amerika na anawaombea baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakati huu wa maandalizi, anawasihi kumsindikiza kwa njia ya sala katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.