2015-06-26 12:20:00

Usilete utani! Mbele ya kifo hakuna fyeke fyeke!


Jamani Maisha ni mfilisi,ukitaka kujua zaidi chungulia Injili ya Mtakatifu Marko:  Mk 5:21-43. Maisha ni kama mchezo wa bao, nchuwa, ajua, sono au engesho. Mshindani wa mchezo anaweza kukufilisi mtaji wako au kukusura kete moja baada ya nyingine hadi unaishiwa zote. Hapo bao limekufa, yaani umefungwa. Aidha, maisha ni kama mfanyabiashara anayefilisika polepole hadi biashara yote inakufa. Ndivyo ilivyo katika safari ya maisha yetu hapa duniani tunafilisika polepole kwa umri, magonjwa, matatizo mbalimbali na kilometa za maisha zinapungua polepole hadi tunafika mwisho wa reli, yaani kifo. Ama kweli maisha ni mfilisi wa uhai wetu.

Ndugu zangu, kufilisika kwa maisha namna hiyo kunalinganishwa na kesi mbili tutakazoziona katika Injili ya leo. Kesi hizi zinaweza kutufungua macho na kutupatia mbinu za kumkabili mfilisi huyo ipasavyo. Katika kesi hizo tutawaona watu wawili wanaofanana kihali na kimatendo. Kwanza kabisa watu hao wanalingana kijinsia, yaani ni wanawake. Hiyo ni jinsia pekee inayoweza kuleta uhai hapa duniani kwa kuzaa. Lakini kwa bahati mbaya, mwanamke wa kwanza hawezi kuzaa kwa vile ana ugonjwa wa kutoka damu.

Kadiri ya fikra za Wayahudi damu ni alama ya uhai, ndiyo maana ni mwiko kwao kula kibudu kwa sababu damu ya kibudu haijachujwa kwani imeganda mwilini. Mwanamke huyu alitokwa damu kwa muda mrefu hali ambayo angedhaniwa si tu amelogwa bali “amepigwa kipapai.” Ugonjwa huu ulimtesa mwanamke huyu kimwili na kumdhalilika kisaikolojia. Mwanamke wa pili ni binti Yairo, aliyeumwa sana na sasa amekufa, na hivi hawezi kuleta uhai hapa duniani. Aidha, katika wanawake hawa kuna namba muhimu kumi na mbili inayojitokeza. Mwanamke wa kwanza alikuwa ametokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, na binti Yairo alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.

Namba hii inawakilisha idadi ya makabila ya Taifa la Waisraeli. Halafu jina hilo Israeli liko katika jinsia ya kike, hali inayowakilisha taifa hilo kuwa ni Mama anayelizalia taifa watoto, lakini kumbe taifa hilo “limepigwa kipapai” kama alivyo mama huyu, yaani taifa linavuja damu, na linaumwa kama binti Yairo na linafilisika taratibu. Kutokana na huluka ya kujilinda uhai wake, binadamu huyo anahangaika kutembea kwa waganga mbalimbali bila mafanikio. Kwa vyovyote binadamu tunamhitaji mmoja anayeweza kutupatia njia ya kutunza na kuendeleza uhai wetu.

Suala jingine muhimu linalofanana katika vituko hivi viwili ni la imani. Mwanamke wa kwanza anaambiwa: “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.” Kwa binti wa pili, neno hilo imani linasikika pale wanapofika wajumbe kumkatisha tamaa Yairo kuwa asiendelee kumsumbua Yesu kwa vile binti yake amefariki, ndipo Yesu anamwambia Yairo: “Usiogope, wewe endelea tu kuamini.”

Baada ya kuziona hali zinazofanana katika kesi hizi mbili, hebu sasa tuyaangalie kinaganaga mazingira ya vituko hivyo. Wiki iliyopita tulisikia kuwa Yesu na mitume wake walienda nchi ya wagerasi (kwa wapagani ng’ambo ya ziwa usiku), na kimbembe walichokipata baharini hawatakaa wakisahau. Sasa wamerudi tena Kafarnaumu. Yesu anapoingizana tu pale kijijini wanamkusanyikia watu kibao: “Akaja mtu mmoja kati ya wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo hata alipomwona, akaanguka miguuni pake.” Mtu mkubwa kama huyu wa Sinagogi kumpigia magoti Yesu ni alama ya unyenyekevu mkubwa.

Ama kweli mbele ya mauti hakuna binadamu wa kufanya fyeke fyeke. Yairo amempa maisha mtoto wake kwa kumzaa. Sasa huluka ya kibinadamu inamsukuma kuutetea mbele ya homa hii kali. Anamsihi Yesu anayeweza kumsalimisha: “Nakuomba uje, uweke mkono wako juu ya binti yangu, apate kupona na kuishi.” Yesu anapoondoka kwenda nyumbani kwa Yairo, njiani anapambana na mama anayetokwa damu. Mama huyu kwa mficho anagusa vazi la Yesu.

Vazi linawakilisha nafsi ya mtu. Kila mmoja anachagua na kuvaa vazi analolitaka kujiwakilisha nafsi na matendo yake alivyo. Angalia mavazi ya watu mbalimbali jinsi yanavyowakilisha jinsia zao, makabila yao hata tabia zao. Vazi la Yesu linawakilisha Nafsi ya Pili ya Mungu yaani Ubinadamu wake. Yesu anapoguswa vazi lake anashtuka na kuuliza: “Ni nani aliyenigusa mavazi yangu?” Mwanamke anafadhaika na kuogopa kwani anadhani anaweza kugombezwa kwa vile ni mchafu. Asijue kwamba Yesu amefika kwa ajili ya watu dhaifu kama yeye.

Baada ya uponyaji huu, Yesu aaendelea na safari kwenda nyumbani kwa Yairo. Akiwa bado njiani watu wanafika kumwambia Yairo: “homa ile imetuacha usimsumbue tena Yesu”. Hao wajumbe wanaamini kwamba Yesu hawezi kufanya kitu zaidi mbele ya kifo. Hapa kuna hatari hata kwa Yairo kupoteza imani. Lakini Yesu anamtia moyo na kumwambia: “Wewe endelea kuamini tu binti yako hajafa, bali amelala” na kulala siyo mwisho bali ni uchovu tu, usingizi ukiisha ataamka na kuendelea na maisha.

Watu wasioamini wanamcheka Yesu anaposema kuwa binti amelala, kwani asiyeamini anaona tu hatima ya maisha haya. Yesu anaingia ndani ya nyumba ya Yairo, anawafukuza wote isipokuwa mitume tu kama mashahidi wa binadamu anayeguswa na Yesu na kupata uhai. Anawabakiza pia wazazi wa binti, kwani wazazi ndiyo wanaoleta uhai hapa duniani kwa kuzaa. Maisha hayo yakiguswa na Yesu yataendelea kudumu.

Yesu “anamshika mkono kijana na akamwambia, Talitha kum; yaani msichana nakuambia inuka.” Ni alama ya maisha yanayopokea mkono wa Mwana wa Mungu (Yesu) na yanamwinua kutoka maisha ya kibaolojia yanayokufa na kumweka katika maisha ya milele yasiyokufa. Kisha Yesu, “akaamuru apewe chakula,” maana yake, maisha hayo mapya aliyotupatia Yesu duniani yanatakiwa yalishwe kwa matendo mema na kwa njia ya Ekaristi Takatifu.

Ndugu zangu, sisi sote tupo daima katika harakati za kuhifadhi au kutetea uhai wetu. Lakini bila kugusa vazi la Yesu aliye uhai, maisha yetu ya kibaolojia yanapotea. Yaani yabidi kuutambua na kuuvaa ubinadamu wake unaowakilishwa na vazi lake. Hapa kila mmoja anaalikwa kuihoji nguo  aliyoitundika mwilini kama inawakilisha utu na ubinadamu wake au la!

Mtume Paulo anasema: “Inabidi kumvaa Kristo aliye nguo mpya.” Kwa hiyo ili tupate kuwa na uzima yatubidi kuugusa kwa unyenyekevu ubinadamu wa Yesu yaani kugusa vazi la Kristu kwa imani kwa njia ya Neno lake yaani Injili. Kugusa kwa imani, maana yake ni kupokea ukweli wa maisha aliyoyapendekeza Yesu na kuyaishi. Tuilishe imani hiyo na matendo yetu mema kwa Sala na kupokea Ekaristi Takatifu. Hapo maisha yetu hayatakuwa mfilisi.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.