2015-06-26 10:16:00

Patriaki Nerses Bedros XIX Tarmoun amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Patriaki Nerses Bedros XIX Tarmoun wa Kanisa la Cilicia ya Waarmeni, aliyefariki dunia hapo tarehe 25 Juni 2015, huko Beirut, Lebanon, akiwa na umri wa miaka 75. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Sinodi pamoja na waamini wote wa Kanisa la Waarmenia, anapenda kuungana nao kwa njia ya sala wakati huu wanapoendelea kuombeleza msiba huu mzito kwa kuondokewa na kiongozi wao mkuu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, anakumbuka jinsi walivyokuwa na ushirikiano wa karibu, kiasi hata cha kumtangaza Mtakatifu Gregori wa Narek kuwa Mwalimu wa Kanisa. Hiki ni kilele cha ushirikiano na umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuiweka roho ya Marehemu Patriaki Nerses Bedros chini ya huruma na upendo wa Mungu, kiongozi ambaye alijisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu aliyokuwa amekabidhiwa kwake.

Ni kiongozi ambaye kama: Padre na Askofu alitekeleza vyema wajibu wake huko Alessandria na baadaye akateuliwa kuwa ni Patriaki wa Kanisa la Cilicia ya Waarmeni. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema walioguswa na msiba huu mzito kwa njia ya sala. Anapenda pia kuwapatia baraka zake za kitume Familia yote ya Mungu na wale wote watakaoshiriki katika mazishi ya Patriaki Nerses Bedros XIX Tarmoun wa Kanisa la Cilicia ya Waarmeni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.