2015-06-26 16:20:00

Maaskofu wakuu 46, kati yao 8 kutoka Barani Afrika kupewa Pallio Takatifu


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia majira ya saa 3: 30 asubuhi.

Baba Mtakatifu atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu watakaporudi majimboni mwao, ili kuonesha mshikamano wa dhati na Familia ya Mungu inayounda Jimbo kuu husika. Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wakuu watavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika.

Maaskofu walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2015 ni 46, kati yao kuna Maaskofu wakuu 8 kutoka Majimbo makuu Barani Afrika. Hawa ni Askofu mkuu Djalwana Laurenti Lompo kutoka Jimbo kuu la Niamey, Niger. Askofu mkuu Jean Mbarga kutoka Jimbo kuu la Yaoundè, Cameroon. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya kutoka Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania.

Wengine ni Askofu mkuu Filomeno do Nascimento Vieira Dias wa Jimbo kuu la Luanda, Angola. Askofu mkuu Martin Musonde Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya. Askofu mkuu Benjamin Ndiaye wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal. Askofu mkuu Menghesteab Tesfamariam, wa Jimbo kuu la Asmara, Eritrea pamoja na Askofu mkuu Juan Nsue Edjang Mayè wa Jimbo kuu la Malabo, Guinea Equitorial. Katika Ibada hii ya Misa takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wanne wametoa taarifa ya kutoweza kuhudhuria na kwamba, Pallio zao watapelekewa na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.