2015-06-26 09:24:00

Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa yanalenga kutoa kipaumbele kwa Familia


Maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Kimataifa yatazinduliwa rasmi kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 27 Septemba 2015 Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani na kwamba, yanaongozwa na kauli mbiu “Upendo ni utume wetu. Familia inauishi kikamilifu”. Hii itakuwa ni fursa makini kuweza kutafakari kuhusu ukweli wa maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo pamoja na kutambua mchango wake katika ujenzi wa jamii.

Haya pia yatakuwa ni maadhimisho ya kifamilia, kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”. Mada mbali mbali zitachambuliwa na hatimaye kufanyiwa kazi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia.

Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, siku ya Alhamisi, tarehe 25 Juni 2015 kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya nane ya familia kimataifa. Mkutano na waandishi wa habari umehudhuriwa pia na Askofu mkuu Charles Joseph Chaput wa Jimbo kuu la Philadelphia, pamoja na Askofu saidizi John McIntyre pamoja na Bwana na bibi Jerry na Lucille Francesco wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu walipofunga ndoa. Wanandoa hawa wametoa salam na matashi mema kutoka kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Philadelphia.

Askofu mkuu Paglia anabainisha kwamba, maadhimisho ya Siku ya nane ya familia kimataifa ni fursa makini inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika jamii kwa ujumla. Wakati wa maadhimisho haya, wanafamilia kutoka sehemu mbali mbali za dunia watashirikisha shuhuda za maisha na utume wa familia, furaha na changamoto wanazokabiliana nazo bila kusahau siri ya mafanikio, iliyowawezesha baadhi yao hata kusherehekea Jubilei ya miaka 25, miaka 50 na hata wengine zaidi ya hapo katika kifungu cha Sakramenti ya Ndoa Takatifu.

Ni wakati wa kuadhimisha na kufurahia  zawadi ya upendo ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu, ili kuwahamasisha waamini na wote wenye mapenzi mema kudumu katika ukweli na uaminifu wa maisha yao ya ndoa na familia, licha ya changamoto na magumu wanayokabiliana nayo katika mchakato wa maisha ya pamoja yanayopania kuwatakatifuza. Ni nafasi ya kushuhudia kwa walimwengu kwamba, kwa hakika familia ni rasilimali muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya mwanadamu.

Mama Kanisa anapenda kuwadhihirishia walimwengu kwamba, familia ni kwa ajili ya mafao ya binadamu na wala si kinyume chake na kamwe familia haiwezi kubinafishwa na dini moja. Kutokana na mantiki hii, Jimbo kuu la Philadephia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, litakuwa ni Makao makuu ya Familia duniani, kwa kushirikisha umati mkubwa wa familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 27 Septemba 2015 atashiriki maadhimisho haya kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baada ya Misa atawakabidhi wawakilishi wa familia kutoka katika baadhi ya miji mikuu Injili ya Luka. Hawa ni wawakilishi kutoka Kinshasa mji mkuu wa DRC kwa niaba ya Bara la Afrika. Avana, Cuba kwa niaba ya Amerika; Hanoi kwa niaba ya Oceania na Marsiglia kwa niaba ya Bara la Ulaya. Nakala millioni moja za Injili ya Luka zitasambazwa sehemu mbali mbali za dunia, hususan kwenye maeneo maskini zaidi, ili kuwasaidia waamini kutambua kwamba, Injili inapaswa kuwa kitabu cha Familia anakaza kusema Askofu mkuu Vincenzo Paglia.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Chaput amefafanua kwa kina na mapana maandalizi yaliyokwishafanyika katika kipindi cha miaka mitatu, tangu Jimbo kuu la Philadelphia lilipoteuliwa kuwa Mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Nane ya familia Kimataifa. Hadi wakati huu zaidi ya watu elfu kumi na mbili wamekwisha jiandikisha ili kushiriki wakati wa maadhimisho haya. Hata majimbo maskini, yamechangiwa ili kuhakikisha kwamba, wanafamilia kutoka katika maeneo haya wanashiriki kikamilifu.

Kuna umati mkubwa wa watu waliojiandikisha ili kushiriki kutoa huduma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa. Itakuwa ni nafasi ya kuzungumzia masuala ya kidini, kitamaduni na kiuchumi na kwamba, tukio hili lina mvuto mkubwa kwa vyombo vya upashanaji habari. Ni maadhimisho ambayo yanatangulia kidogo Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, kumbe, haya ni matukio yanayokwenda bega kwa bega ili kuonesha umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu msaidizi McIntyre anasema kwamba, kila siku kutakuwa na nada kuu mbili zitakazotolewa na waamini kutoka katika dini na mataifa mbali mbali, wote watazungumzia uzuri na utakatifu wa maisha ya familia. Itakuwa ni fursa kwa familia kuweza kusikiliza tafakari kuhusu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu kuhusiana na utunzaji bora wa mazingira “ Laudato si” yaani, “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa nyumba ya wote”. Hapa familia zinahamasishwa kulinda na kutunza mazingira.

Waraka wa kitume wa Mwenyeheri Paulo VI, “Humanae vitae”, yaani “Maisha ya binadamu” utachambuliwa kwa kina na mapana, ili kweli familia ziweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Washiriki wa maadhimisho haya watapata muda wa kusali, kujadiliana na kubadilishana mawazo. Baba Mtakatifu Francisko atashiriki pia mkesha wa siku ya familia kimataifa, Jumamosi, tarehe 26 Septemba 2015. Siku hii itapambwa pia kwa muziki unakaoporomoshwa na Andrea Bocelli, mwimbaji mashuhuri kutoka Italia. Ni tukio ambalo linatarajiwa kuwashirikisha watu zaidi ya millioni moja.

Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, tangu kuanzishwa kwake, yamefanyika: Roma, kunako mwaka 1994, Rio de Janeiro, Brazil mwaka 1997, Roma, Italia, wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Jimbo kuu la Manila kunako mwaka 2003; Jimbo kuu la Valencia, Hispania, mwaka 2006 na Mexico city, nchini Mexico, mwaka 2009, mwishoni ni Jimbo kuu la Milano, Italia, kunako mwaka 2012.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.