2015-06-25 16:15:00

Onesheni mshikamano na Papa Francisko kwa kuchangia huduma ya upendo!


Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro Paulo, miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni ni siku ambayo pia, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kwa namna ya pekee kuonesha upendo na mshikamano na Baba Mtakatifu kwa kuchangia kwa hali na mali katika huduma ya upendo inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa maskini na wahitaji zaidi, kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kuonja huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huduma ya upendo ni ushuhuda madhubuti unaopaswa kuwa ni utambulisho wa wafuasi wa Kristo popote pale walipo. Upendo huu, uwaguse na kuwatambulisha miongoni mwa Watu wa Mataifa.

Hii ni changamoto inayotolewa na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Roma katika barua yake kwa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Roma. Mchango makini kwa huduma ya upendo unaotekelezwa na Baba Mtakatifu ni fursa inayowawezesha waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kutambua dhamana na mchango wa Kanisa katika kuwamegea watu huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyokaza kusema katika Waraka wake wa kichungaji kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kutokana na kuota sugu utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, watu wengi wanajikuta wakitumbukia katika tabia ya kubeza watu, mambo ambayo yanaufanya moyo kuwa mgumu kama “jiwe” hali inayopelekea utepetevu unaoharibu maisha ya watu.

Kardinali Vallini anawaalika viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawafafanulia waamini wao kuhusu umuhimu wa siku hii na mchango wao wa hali na mali katika kusaidia mchakato wa utangazaji wa Injili ya upendo kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa waamini wa Jimbo kuu la Roma, wanawajibu mkubwa zaidi. Tangu wakati huu, Kardinali Vallini anapenda kuwaweka waamini wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria afya ya Warumi pamoja na kuwapatia baraka zake za kichungaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.