2015-06-25 15:57:00

Nendeni mjifunze mahangaiko ya watu kwa kusikiliza kilio cha damu!


Shirika la Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu kwa namna ya pekee mwaka huu linaadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu Shirika hili lilipoanzishwa na Mtakatifu Gaspar del Bufalo kunako tarehe 15 Agosti 1815, huko Giano, dell’Umbria, nchini Italia. Kilele cha Jubilei hii ni hapo tarehe 1 Julai 2015, Familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia itakapokusanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano mjini Roma, ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani.

Tukio hili linatarajiwa pia kuhudhuriwa na mahujaji kutoka Tanzania, wenye ibada kwa Damu Azizi ya Kristo, mto wa rehema na chombo cha upatanisho, haki na amani. Hija hii itajikita katika maisha ya toba na wongofu wa ndani, kwa kutembelea maeneo ambayo yana historia na kumbu kumbu za Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Italia. Katika maadhimisho haya, Padre Ernest Gizzi ambaye kwa miaka mingi alifanya kazi na utume wake nchini Tanzania, ataadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya Upadrisho.

Nchini Tanzania, Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 26 Juni 2015 wanaendesha Juma la Damu Azizi ya Yesu, fursa ya kuangalia tasaufi, historia, changamoto na matarajio ya Shirika nchini Tanzania, wakati huu wanapojiandaa kuzindua rasmi Kanda mpya ya Tanzania hapo mwezi Agosti, 2015. Maadhimisho haya Juma la Damu Azizi ya Yesu yanaongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya miaka 200 ya Umissionari katika Shirika la Damu Azizi ya Yesu; maisha ya kitawa na tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu”.

Mada ambazo zimechambuliwa wakati huu ni kuhusiana na maana ya Jubilei mintarafu Biblia; Ndoto za Mtakatifu Gaspar za kutaka kueneza Ibada ya damu Azizi ya Yesu hadi miisho ya dunia; Maisha ya kitawa na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo bila kusahau changamoto zinazoendelea kulikabili Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu.

Katika mahubiri yake, kwenye uzinduzi wa Juma la Damu Azizi ya Yesu, Padre Reginald Mrosso, Mkuu wa Shirika, Vikarieti ya Tanzania, amebainisha umuhimu wa damu katika maisha ya binadamu na kwamba, wanashirika wanatumwa na kuhamasishwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni Manabii kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na upatanisho.

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wajitahidi kumwilisha dhana ya unabii na umissionari katika maisha na utume wao miongoni mwa watu wa Mungu, kwa kuendelea kuiga mfano wa Mtakatifu Gaspar aliyejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, kiasi hata cha kukubali kupelekwa uhamishoni. Ni kiongozi aliyewasaidia watu wa Sonino kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya upatanisho. Kwa njia ya mahubiri na mfano bora wa maisha yake, watu wengi waliguswa na neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakatubu na kumwongokea Mungu, kwani daima alitamani kuokoa roho za watu na wala si kuziangamiza.

Huu ni mwaliko kwa Familia ya Mtakatifu Gaspar kuhakikisha kwamba inaiga mfano wa maisha na utume wa Mtakatifu Gaspar kwa ajili ya watu wa nyakati hizi, ambao wanabeba ndani mwao madonda makubwa ya chuki, utengano na uhasama. Walisaidie Kanisa kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho kama ambavyo wanakaza kusema Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.

Padre Reginald Mrosso anawataka Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, kuwa wepesi kusikiliza na kujibu kilio cha Damu Azizi ya Yesu, kinachoendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia. Wasukumwe na upendo wa Kristo unaowawajibisha kwenda hata zile sehemu ambazo zinaonesha utata.

Katika kipindi cha miaka kumi ijayo, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania linataka kujielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo, kwa kuwashirikisha Injili ya Furaha kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Dira na mwelekeo huu utaweza kuzaa matunda kwa njia ya utamadunisho, umoja na mshikamano wa kidugu unaoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha.

Na Rodrick Minja kutoka Dodoma.

Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.