2015-06-25 08:36:00

Mhudumu wa maskini na wanyonge, amepumzika katika usingizi wa amani!


Sr. Nirmala Joshi, Mama mkuu mstaafu wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta, amefariki dunia siku ya Jumanne, tarehe 23 Juni 2015, akiwa na umri wa miaka 81 kutokana na ugonjwa wa moyo. Marehemu Sr. Nirmala Joshi amezikwa kwenye makaburi ya Nyumba mama ya Shirika, jumatano tarehe 24 Juni 2015. Itakumbukwa kwamba, Sr. Nirmala Joshi alikuwa ni Mama mkuu wa kwanza baada ya Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta.

Kwa muda mrefu Sr. Nirmala Joshi alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo, Ijumaa tarehe 19 Juni 2015 hali yake ikawa mbaya na madaktari wakashauri kwamba, alazwe, ili aweze kufanyiwa uchunguzi na matibabu makubwa zaidi, lakini, Sr. Nirmala, alipenda kubaki na watawa wenzake. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sr. Nirmala alirudishwa kwenye Jumuiya na huko baadaye alikata roho.

Sr. Nirmala Joshi alizaliwa kunako mwaka 1934 huko Ranci, mji mkuu wa Jharkanda, huko India. Licha ya wazazi wake kuwa waamini wa dini ya Kihindu, lakini alibahatika kupata elimu kutoka katika shule za Kikatoliki. Akiwa shuleni alibahatika kuona na kushuhudia kazi kubwa ya upendo iliyokuwa ikitekelezwa na Mama Theresa wa Calcutta, kiasi cha kuvutiwa kujiunga na huduma hii kwa ajili ya maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Akabatizwa na baadaye akajiunga na Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta. Alikuwa ni mtaalam katika masuala ya sayansi jamii na mwanasheria, akawa ni mtawa wa kwanza kuongoza kundi la watawa katika nchi za kimissionari huko Panama. Kunako mwaka 1976, Sr. Nirmala akaanzisha tawi la watawa wa upendo waliokuwa wanajikita katika tafakari zaidi.

Kunako mwaka 1997 akachaguliwa kuongoza Shirika na miezi sita baadaye, Mama Theresa wa Calcutta, akafariki dunia. Ni mtawa alipenda kujisadaka zaidi katika maisha ya tafakari na huduma kwa maskini. Tareghe 25 Machi 2009 akamaliza muda wake wa uongozi kama Mama mkuu wa Shirika na kupokelewa na Sr. Mary Prema Pietrick, kutoka Ujerumani, ambaye hadi sasa ndiye Mama mkuu wa Shirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.