2015-06-25 15:10:00

Iweni watu wa huduma katika mapendo kwa njia ya unyenyekevu pasi na makuu


Kipindi cha masomo na maisha ya kijumuiya ni muda muafaka kwa ajili ya kuwafunda wakleri katika huduma ya kidiplomasia inayotekelezwa na Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Kuna kundi kubwa la watu ambalo limeshiriki katika kuwafunda wahudumu hawa wa Kanisa katika maisha ya: kitamaduni, kiroho pamoja na kuratibu mchakato mzima wa maisha katika taasisi ya kidiplomasia ya Kanisa, changamoto ya kusonga mbele kwa furaha katika hija hii ya maisha.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 25 Juni 2015 kwa Jumuiya ya Taasisi ya Kidiplomasia ya Kanisa, wakati huu inapofunga mwaka wa masomo, tayari kutumwa sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa utume unaowaandaa kwa namna ya pekee kabisa kuwa ni wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia, kwa kutambua kwamba, Kanisa la Roma ni msingi wa huduma ya upendo, changamoto na mwaliko wa kuonesha unyenyekevu pasi na kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mamlaka ya Kanisa Katoliki yanajikita katika upendo wa Kristo, nguvu inayowawezesha kuaminiwa na watu wa mataifa; ni nguvu ya ukweli inayobomoa kuta za utengano, ili kujenga madaraja ya umoja kati ya watu. Hii ndiyo siri ambayo imefichama katika utume unaoboreshwa kwa njia ya matumaini ambayo kamwe hayatambui hali ya mtu kushindwa.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, wawakilishi wa Vatican si wafanyakazi wa Serikali wala kundi la wateule, bali ni walinzi na watetezi wa ukweli unaopaswa kuhifadhiwa katika kumbu kumbu zao bila ya kumezwa na ugumu wala utepetevu wa moyo, bali mashuhuda amini wa uso wa Baba yao wa mbinguni, anayewaongoza katika hija ya maisha yao kwa njia ya sauti yake.

Majiundo makini yanayotolewa kwenye Taasisi ya Kidiplomasia ya Kanisa, yanawasaidia kwa namna ya pekee kuwaandaa ili kuwa ni madaraja ya amani yanayojengwa kwa njia ya sala na mapambano ya maisha ya kiroho; kwa kujinyenyekesha pasi na kutaka makuu au wakati mwingine kujivika vinyago vinavyowafanya kushindwa kuonesha ile sura halisi ya maisha yao kwa kudhani kwamba, wanafahamu mambo mengi zaidi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huduma wanaotumwa kuitekeleza inawataka kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa Vatican, ili iendelee kuwa aminifu kwa wito wake mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya mafao ya wengi. Wasikubali kutekwa na kufungwa katika siasa na mantiki zitakazowafanya kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Daima walitafute Kanisa na watu katika maeneo wanamoishi na kuhudumiwa; watafute mema yanayopaswa kudumishwa.

Ili kutekeleza vyema dhamana hii, kamwe wasiwe ni mahakimu, bali walimu watakaolisaidia Kanisa pamoja na viongozi wake kushuhudia ile nguvu ambayo Mwenyezi Mungu ameipandikiza ndani mwao. Wawe tayari kuandaa mazingira kwa njia ya mikono yao wenyewe, huku wakiendelea kusubiri kwa unyenyekevu ili Mwenyezi Mungu aweze kutenda kazi yake na pengine, wao hawataweza kuvuna wala kufaidi matunda ya kazi kubwa waliyoifanya. Wawe na ujasiri wa kuthubutu kuonesha kipaji cha ugunduzi na kamwe wasiridhike na kazi iliyofanywa na watangulizi wao.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro wanaowajibu wa kutafuta wachungaji waaminifu na wakweli, wanyenyekevu na wachamungu; wadumifu katika maisha na utume wa Kanisa; hawa wapo na kamwe Mwenyezi Mungu hachoki kulipatia Kanisa watu kama hawa. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanaangalia yale yaliyofichika moyoni mwa watu na wala si mambo ya nje. Wawe na ujasiri wa kutafuta watu wa Mungu, kwa kushirikiana na wale ambao wamedhamiwa kwao na Kanisa. Wawe na uhakika wa maamuzi wanayofanya hata kama kutakuwa na wasi wasi.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wawakilishi wa Vatican kwamba, iko siku watatumwa sehemu mbali mbali za dunia. Bara la Ulaya linahitaji kuamshwa tena; Afrika ina kiu ya upatanisho; Amerika ya Kusini inahitaji lishe bora na undani wa maisha; Amerika ya Kaskazini, watu wanataka kugundua utambulisho wao unaowakumbatia wengine badala ya kuwatenga; Barani Asia na Oceania: changamoto ni kudhibiti hali ya kujisikia kuwa wako diaspora pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya tamaduni za wahenga.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo tafakari ambayo amependa kuwaachia wakati huu wanapohitimu masomo na majiundo yao, tayari kwenda kutekeleza utume sehemu mbali mbali za dunia. Anawataka kamwe wasikubali kukatishwa tamaa na matatizo pamoja na changamoto za maisha watakazokumbana nazo. Daima watambue kwamba, watapata msaada kutoka kwa Yesu Kristo. Bikira Maria, awasaidie na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, ili waweze kulipenda Kanisa. Watambue kwamba, maisha yao yote ni kwa ajili ya huduma ya Injili na Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.