2015-06-24 15:51:00

Onesheni ushupavu; dumisheni upendo mkuu, iweni watu wa imani na matumaini!


Maadhimisho ya Siku kuu ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji, sherehe inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, yamehitimisha pia Onesho la Sanda Takatifu lililokuwa linafanyika Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia; tukio ambalo limehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, katika mahubiri yake kama ujumbe mahususi kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino amekazia mambo makuu yafuatayo: ushupavu katika ushuhuda; umuhimu wa kushuhudia upendo mkuu; waamini wameimaarishwa katika imani na Baba Mtakatifu, sasa ni wakati wa kuzaa matunda yanayokusudiwa; waamini waangalie mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa, wakitambua kwamba, Mtakatifu Yohane Mbatizaji msimamizi wa Jimbo lao anawaongoza na kuwasimamia, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino, inapaswa kuwa ni kielelezo makini cha ushuhuda wa umoja na udugu; kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; kwa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu, ili kuondokana na ubinafsi pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Waamini wawe ni wajumbe wa imani, matumaini na mapendo kati ya watu wanaowazunguka. Wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kimaadili katika maisha binafsi na hadharani, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa kijamii na kitamaduni.

Onesho la Sanda Takatifu Jimbo kuu la Torino, ilikuwa ni nafasi ya kushuhudia upendo mkuu uliopelekea Yesu, akateswa, akafa na hatimaye, kufufuka kutoka kwa wafu, changamoto ya kukumbatia, kuenzi na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wawe kweli ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa njia ya huduma ya upendo na sadaka. Jubilei ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco iendelee kushuhudia utajiri mkubwa wa kiutu na maisha ya kiroho.

Askofu mkuu Cesare anasema kwamba, Familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino, imeimarishwa na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye amewezesha umati mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali nje ya Jimbo kuu la Torino kufika na kushuhudia matendo makuu ya Mungu. Waamini wanapaswa wakati huu kufanyia kazi mafundisho makuu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji Jimboni humo. Waimarishe mshikamano wa udugu, wawe na ujasiri wa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wawaonjeshe upendo maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia anaitaka Familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino kuhakikisha kwamba, inakuwa na imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kutumia karama, vipaji na nguvu iliyomo ndani mwao, ili kusaidia mchakato wa maboresho katika maisha, kila mtu akiwa tayari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kujenga na kuimarisha haki, usawa na mshikamano. Mtakatifu Yohane Mbatizaji, msimamizi wa Jimbo kuu la Torino, awe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.