2015-06-24 15:36:00

Ondoeni mawazo mgando, ponyeni majereha na jengeni utamaduni wa kusikilizana!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya katekesi yake kwa siku ya Jumatano, tarehe 24 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki mkutano wa majadiliano ya kidini kati ya Wabudha na Wakatoliki kutoka Marekani, tukio ambalo limeandaliwa na Chama cha Fokolari kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Tume ya majadiliano ya kidini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Baba Mtakatifu katika salam zake, amewapongeza wajumbe hawa kwa kumtembelea na kwamba, anawashukuru kwa moyo wake wote kwani hizi ni dalili za udugu, majadiliano na urafiki, mambo msingi yanayoweza kudumisha ushuhuda wa pamoja miongoni mwa waamini. Historia ya nyakati hizi imesheheni madonda ya chuki, uhasama na vita, kumbe, matukio kama haya ni mbegu ya amani na udugu.

Kwa upande wake, Kardinali Jean Luis Tauran, Rais wa Baraza la kipapa la majadiliano ya kidini katika hotuba yake ya ufunguzi kwa wajumbe wa mkutano huu, hapo tarehe 23 Juni 2015 anakaza kusema, uwepo wao ni changamoto ya kukuza na kudumisha udugu na urafiki. Mkutano huu unaofanyika huko Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, unaongozwa na kauli mbiu: mateso, ukombozi na udugu. Mkutano huu unatarajiwa kuhitimishwa, Jumamosi, tarehe 27 Juni 2015.

Huu ni mkutano unaowashirikisha wajumbe wa dini ya Kibudha kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Jean Louis Tuaran anasema kwamba, Waraka wa kitume uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano ya kidini,  yaani “Nostra aetate” unaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50, mwaliko wa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini kwa kutegemea mwanga na baraka kutoka juu.

Waamini wote watambue kwamba, hapa duniani ni mahujaji na wala hawana makazi ya kudumu. Kumbe, majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wabudha yanapania pamoja na mambo mengine kufanya tafakari ya pamoja kuhusu Fumbo na Kweli za maisha. Ili kuweza kufikia hatima ya hija hii, anasema Kardinali Tauran, kuna haja kwa waamini kujikita katika mambo makuu matatu: Kwanza kabisa kuondokana na mawazo mgando, kuganga na kuponya madonda; woga na wasi wasi, tayari kujenga utamaduni wa kusikilizana kwa dhati.

Pili anasema Kardinali Tauran, waamini wajitahidi kujenga madaraja yanayowakutanisha watu kutoka katika kila kabila, lugha na jamaa; tayari kufahamiana, kuheshimiana na kusaidiana katika hija ya maisha, kwani wote ni wapita njia na hawana makazi ya kudumu. Hapa waamini wa dini mbali mbali wajenge urafiki kwa njia ya ukarimu, ili kuondoa ujinga unaowajengea hofu na wasi wasi zilizokuwa na msingi wala mashiko, ili kweli mapatano yaweze kuota mizizi katika akili na mioyo ya watu.

Kardinali Tauran anakaza kusema, hatua ya tatu ni waamini wanapojerea makwao, wakitahidi kumwilisha uzoefu na mang’amuzi waliyoyapata katika hija ya maisha yao, kwa kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kidini ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; daima wakitafuta mafao ya wengi, ili kujenga na kuimarisha udugu wa kweli.

Ni matumaini ya Kardinali Tauran kwamba, siku tano za sala, tafakari, kusikilizana na kushirikishana, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga na kudumisha mchakato wa umoja na udugu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya binadamu.

Kwa upande wake,  Donald W. Mitchell, mratibu wa mkutano huu anasema kwamba, majadiliano ya kidini yanapania kujikita katika kuangalia chanzo na sababu zilizopelekea uwepo wa madonda na mipasuko ya kidini na jinsi ambavyo wanaweza kwa kushirikiana kwa pamoja, kutibu na kuganga madonda haya kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Majadiliano ya kidini yasaidie kuimarisha umoja na ushirikiano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali, ili kuendeleza mchakato wa misingi ya haki, amani na upatanisho, ili watu waweze kujenga umoja na udugu.

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.