2015-06-24 15:20:00

Kinzani na misigano ya kifamilia, waathirika wakuu ni watoto!


Baba Mtakatifu Francisko katika mfululizo wa Katekesi zake kuhusu Familia kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Familia amechambua mada mbali mbali zinazohusiana na maisha pamoja na utume wa Familia. Amegusia udhaifu wa kibinadamu unaojitokeza ndani ya familia; umaskini, magonjwa na kifo kinapoitikiza misingi ya familia.

Siku ya Jumatano, tarehe 24 Juni 2015, Baba Mtakatifu amezungumzia pale familia yenyewe inapotendeana mabaya, jambo ambalo linahuzunisha na kusikitisha kabisa, kwani hapa wanafamilia wanakosana kwa maneno, kwa mawazo na kwa kutotimiza wajibu, kiasi cha kuchukiana, kudhalilishana na kuonesha ubabe na umame; matokeo yake ni wanafamilia kutafuta faraja nje ya familia, bila kufikiria mafao ya familia nzima, hususan watoto ambao kimsingi ndio waathirika wakubwa wa patashika nguo kuchanika kayi ya wazazi

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wanandoa wanapoficha madonda na mipasuko katika maisha yao, wanaikuza na matokeo yake ni kusambaratika kwa familia. Wanandoa wakumbuke kwamba, wao ni mwili mmoja na roho moja; madonda na machungu ya utengano kati ya wanandoa, yanawagusa na kuwaathiri sana watoto. Yesu alikwishawaonya watu wazima wasiwe ni kikwazo kwa watoto wadogo, kwa kutambua wajibu na dhamana ya kulinda na kudumisha agano la ndoa, msingi wa maisha ya familia ya binadamu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba, hata kama madonda na misigano kama hii inaweza kusababisha wanandoa kutengana, bado kuna waamini wanaoendelea kubaki kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa; kwa kujikita katika imani na upendo wa dhati kwa watoto wao. Kwa wale wanaojikuta wakitumbukia katika mahusiano tenge, Kanisa halina budi kutafuta njia ya kuwasaidia na kuwaongoza katika hija ya maisha yao ya kiroho.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Yesu Kristo awasaidie kuwa na imani thabiti, ili kwa macho yake waweze kuona ukweli wa maisha na utume wa Familia; kwa kudumisha upendo wa dhati nda ni ya familia. Waamini wajitahidi kuziendea familia zote kwa moyo wa huruma na mapendo. Katika shida na magumu ya maisha, wanafamilia wamkimbilie Yesu, ili aweze kuwaganga na kuyaponya madonda yao, ili nao waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Waamini waoneshe upendo unaomwilishwa katika matendo kwa familia ambazo zinaogelea katika shida na magumu mbali mbali ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaomba waamini kuendelea kuziombea familia ambazo zimesambaratika baada ya kukumbwa na dhoruba kubwa ya maisha, ili ziweze kupata mwanga ule uliowaangazia walipokutana kwa mara ya kwanza katika maisha yao. Familia za namna hii, zitambua mateso na mahangaiko ya watoto wao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waendelee kuimarisha mahusiano mema ndani ya familia zao, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Familia, Uhai na Mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Familia zijenge utamaduni wa kushiriki mara kwa mara Ibada ya Misa Takatifu, ili kujichotea nguvu ya kuweza kukabiliana na mitikisiko katika maisha ya ndoa na familia. Familia zioneshe ushuhuda kwa njia ya matendo ya huruma, kwa kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Katekesi na matukio kama haya ya Kikanisa, yatasaidia kwa namna ya pekee kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa tarehe 24 Juni ya kila mwaka, linaadhimisha Siku kuu ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, aliyemwandalia Yesu njia na kumtambulisha kwa watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema Yohane Mbatizaji aweze kuwa kweli ni mfano wa ujasiri kwa ajili ya mema, daima waungane na Yesu, katika shida na mahangaiko yao pamoja na kudumisha upendo kwa familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.