2015-06-24 16:04:00

Diplomasia ya Vatican inakazia: utu na heshima ya binadamu na uhuru wa kuabudu


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, diplomasia ya Vatican inapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbali mbali za kimataifa.

Kardinali Parolin ameyasema hayo, Jumanne tarehe 23 Juni 2015 wakati alipokuwa anashiriki katika kongamano la kimataifa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu  Jumuiya ya Kimataifa ilipoweka sahihi mkataba wa Helsinki. Tukio hili limwefunguliwa na Bwana Pietro Grasso, Rais wa Senate ya Italia, kwenye ukumbi wa Senate ya Italia, mjini Roma. Kardinali Parolin anakiri kwamba, hata leo hii, uhuru wa kidini bado unakabiliwa na changamoto kubwa sehemu mbali mbali za dunia.

Vatican itaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kidini kwa watu wote pasi na ubaguzi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, Wakristo ni kati ya makundi ya kidini ambayo yanakabiliwa na dhuluma, nyanyaso na hata mauaji, kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, hata Wakristo wanalindwa dhidi ya misimamo mikali inayofanywa dhidi yao.

Ikumbukwe kwamba, uhuru wa kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kiini cha mchakato wa haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Majadiliano katika misingi ya ukweli, uwazi na mafao ya wengi ni nyenzo msingi katika kufikia amani ya kudumu pamoja na kudumisha haki msingi za binadamu. Kardinali Parolin anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, haki za wahamiaji na wakimbizi zinalindwa, kwani hata kama ni wageni, hali hii haiwezi kufuta utambulisho wao kama sehemu ya Familia kubwa ya binadamu.

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Jumuiya ya Kimataifa ilipoweka sahihi mkataba wa Helnsinki, iwe ni fursa makini ya kulinda na kudumisha misingi ya nyumba ya wote pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa nyumba hii kwa ajili ya mafao ya wengi, dhidi ya utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao. Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si mikakati na sera za kiuchumi.

Kardinali Parolin anasema kwamba, mahali ambapo uhuru wa kidini unasimamiwa na kudumishwa kikamilifu, hapo mafao ya wengi yanaendelezwa na kwamba, huu ni mwanzo wa ujenzi wa jamii inayojikita katika umoja, udugu na mshikamano, kwa kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hiki ni kielelezo cha mshikamano wa upendo.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anahitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II katika hija yake ya kichungaji nchini Finland, kunako mwaka 1989, alisikika akisema, Kanisa litaendelea kushirikiana bega kwa bega na Jumuiya ya Kimataifa katika kudumisha uhuru wa kidini kwani hii ni sehemu ya utume wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, Hati ya Mkataba wa Helsinki ni ujumbe wa matumaini kwa wananchi wengi wa Bara la Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.