2015-06-23 15:48:00

Hati ya kutendea kazi kwa ajili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia!


Changamoto, wito na utume wa familia ndiyo mambo makuu yanayoongoza Hati ya kutendea kazi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, ijulikanayo kama “Instrumetum Laboris” iliyozinduliwa mjini Vatican, Jumanne, tarehe 23 Juni 2015. Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia itaadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Hati ya kutendea kazi iliyochapishwa inabeba hati elekezi iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu mara baada ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia iliyofanyika mjini Vatican kunako mwezi Oktoba 2014. Hati hii pia imeboreshwa kwa kuongezewa muhtasari wa majibu ya maswali dodoso yaliyotolewa na kujibiwa katika kipindi cha mwaka mmoja na hatimaye, kuhaririwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Kanisa zima.

Hati ya kutendea kazi, yaani Instrumentum Laboris ni mwendelezo wa kazi kubwa iliyofanywa na Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kunako mwaka 2014 na kwamba, inabeba pia mambo nyeti yaliyojadiliwa katika namba 52, 53 na namba 55 mintarafu mchakato wa Kanisa kutaka kuwapatia wanandoa waliotalakiana nafasi ya kushiriki tena Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na kuwaonesha umoja na mshikamano watu wenye mielekeo ya kutaka kuwa na ndoa za jinsia moja, mada ambayo ilionesha mpasuko mkubwa kati ya Mababa wa Sinodi.

Hati elekezi kutoka kwa Mababa wa Sinodi inakazia kwa namna ya pekee kabisa dhana ya familia inayoundwa kwenye msingi wa dhati kati ya bwana na bibi, kwa kuonesha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, lakini pia kwa kuwa na mwelekeo wa uvumilivu na wa dhati kwa familia ambazo zimekumbwa na majereha. Hati hii inabainisha kwamba, mahusiano ya watu wa jinsia moja hayawezi kulinganishwa na ndoa kati ya bwana na bibi na kwamba, ni jambo ambalo halikubaliki na Mababa wa Sinodi.

Mababa wa Sinodi waliendelea kubainisha kwamba, kulikuwa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, mchakato wa kutengua ndoa unafanywa bure uendelee taratibu pamoja na kuwa makini na mchakato wa kuwasili watoto. Mababa wa Sinodi waliangalisha hatari za picha za ngono pamoja na matumizi tenge ya mitandao ya kijamii, kwani watoto na wanawake ndio waathirika wakubwa wa nyanyaso hizi zinazofanywa kwenye mitandao ya kijamii.

Majibu yaliyotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia yameongezwa na kunyambulishwa kwenye Hati ya kutendea kazi, kama sehemu ya mchango wa waamini walei, vyama vya kitume, taasisi na vyuo vikuu. Hati hii mpya imegawanywa sehemu kuu tatu: kusikiliza changamoto kuhusu familia; mang’amuzi ya wito wa familia na utume wa familia nyakati hizi.

SEHEMU YA KWANZA: KUSIKILIZA CHANGAMOTO KUHUSU FAMILIA

Hati hii inabainisha kwamba, idadi ya ndoa zinazofungwa kiserikali na kidini inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka, jambo ambalo limethibitishwa na Mabaraza ya Maaskofu pamoja na familia zenyewe. Idadi ya ndoa zinazovunjika na watu kutalakiana zinaendelea kuongezeka maradufu na kwamba, idadi ya watoto wanaozaliwa inapungua pia kutokana na vijana wa kizazi kipya kushindwa kufanya maamuzi machungu katika maisha yao kwa kuunda familia, hali inayoonesha kinzani katika tamaduni za nyakati hizi pamoja kuwepo kwa kinzani za utambulisho wa mtu binafsi na mahusiano ya ndani ambayo yanapaswa kujikita katika utofauti wa kijinsia kati ya bwana na bibi.

Kuna baadhi ya watu wanaotaka kutambua mahusiano ya watu wa jinsia moja kuwa ni sawa na ndoa. Hapa Mababa wa Sinodi wanataka waamini kufanya maboresho makubwa yanayojikita katika utu na utamaduni na wala si tu katika masuala ya kibaiolojia kuhusiana na tofauti za kijinsia, kwani kushindwa kutambua tofauti za kijinsia ni tatizo kubwa na wala si suluhu ya changamoto iliyopo.

Hati ya kutendea kazi inaendelea kubainisha kinzani na misigano inayojitokeza katika jamii, kiasi cha kubomoa misingi ya maisha ya ndoa na familia. Kati ya mambo haya ni: vita, uhamiaji, matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, ukosefu wa fursa za ajira, umaskini, michezo ya kamari; utamaduni wa kutumia na kutupa; sera na uchumi tenge kuhusiana na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi kwamba, familia hazitengewi rasilimali ya kutosha katika utekelezaji wa majukumu na dhamana yake.

Hapa kuna haja ya kuwa na sera pamoja na mikakati makini itakayosaidia ustawi na maendeleo ya familia. Hapa pia kuna haja ya kuwakumbuka watu wanaotengwa na kubaguliwa katika sera na mikakati ya kiuchumi, inayoacha athari kubwa kwa watoto, wanaokosa mahitaji yao msingi, hawa baadaye ndio wanaokuwa yatima wa kijamii.

Hati ya kutendea kazi inapenda kukazia umuhimu wa familia kama chombo kinachowashirikisha watu, hasa wajane na wazee kwa kuwapatia utu na matumaini; bila kuwasahau walemavu wanaopaswa kusindikizwa ili kukabiliana na mitazo ya kibaguzi wanayokabiliana nayo. Hati hii inajadili kwa kina na mapana familia ambazo zina watoto walemevu kwa kuangalia hatima ya watoto hao mara baada ya wazazi wao kutoweka hapa duniani. Watoto hawana budi kuhakikishiwa usalama na ubora wa maisha.

Hati inaelekeza umuhimu wa Kanisa kuibua mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia za wahamiaji ambazo zinakumbana na madonda makubwa katika safari ya maisha yao, hasa pale wanapokosa  kuonja ukarimu kwa nchi wahisani na haki zao kushindwa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Mambo haya yanaweza kuchochea misimamo mikali ya kidini na kutokubali utamaduni wa jamii inayowapokea wahamiaji na wakimbizi. Mateso na mahangaiko ya wahamiaji haramu yanazidi kuongezeka kila kukicha, kutokana na kukua kwa biashara haramu ya binadamu katika ngazi ya kimataifa.

Hati ya kutendea kazi inathibitisha dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa. Inakumbusha kurasa chungu ambazo wanawake wanakabiliana nazo yaani: nyanyaso, utoaji mimba, kuhasiwa kwa nguvu; kutungishwa mimba kwa ajili ya fedha bila kusahau bidhaa za kuzuia na kutoa mimba ambazo walengwa wake wakuu ni wanawake na wasichana. Kuna watu wenye hamu ya kutaka kupata watoto kwa gharama yoyote ile. Hati inawataka waamini kutambua na kuheshimu maamuzi yanayotolewa na viongozi wa Kanisa; waamini wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika vikao vya maamuzi yanayotolewa na Serikali pamoja na taasisi mbali mbali.

Hati ya kutendea kazi inaonesha mageuzi makubwa yaliyofikiwa na bayoteknolojia kiasi cha kuweza kuchezea viini tete, hali ambayo inaonesha kwamba, binadamu anaweza kutengenezwa kwenye maabara; mambo ambayo yanapingana na mafundisho ya Kanisa. Watu wa namna hii wako mbali na Kanisa, lakini watambue kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu na Kanisa linawaangalia kwa jicho la huruma.

SEHEMU YA PILI: MANG’AMUZI YA WITO WA KIFAMILIA

Hati ya kutendea kazi inakaza kuhusu utimilifu wa maisha ya ndoa unaojidhihirisha katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu inayojikita katika udumifu kwani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala jambo lililotungwa na binadamu. Katika nyakati kama hizi ambazo kuna utepetevu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba linatangaza na kushuhudia matumaini kwa watu wa ndoa kwa kutambua kwamba, Kanisa kamwe haliwezi kiwatelekeza. Umoja na uumbaji ni mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia mintarafu ushiriki wa kazi ya uumbaji inayowajibisha.

Familia inapaswa kuwa ni kiini cha Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa Injili ya Familia unaojikita katika imani tendaji, mshikamano na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kulinda na kutunza mazingira; daima wakitafuta mafao ya wengi. Familia zinahamasishwa kujikita katika mchakato wa katekesi ya familia, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake msingi. Familia ziwe ni mahali pa makuzi katika mchakato wa hija ya imani.

Kanisa na Familia zinategemeana na kutegemezana, changamoto kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinawasaidia wanandoa wanaokumbana na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Familia ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ni wajibu wa Kanisa kuendelea kuwasindikiza wanandoa wanaoogelea katika shida na magumu ya maisha, ili waweze kupata suluhu ya maisha, kwani madhara ya kinzani na misigano kati ya wazazi yanaathari kubwa kwa watoto.

Hati hii inahitimisha sehemu ya pili kwa kukumbusha kwamba, Kanisa litaendelea kujikita katika huruma kwa kukuambata kweli za imani mintarafu ufunuo wa utambulisho wa Mungu na ushuhuda wa utambulisho wa Kikristo.

SEHEMU YA TATU: UTUME WA FAMILIA NYAKATI HIZI

Sehemu ya tatu kimsingi inakazia umuhimu wa kuwaandaa, kuwafunda na kuwawajibisha wanandoa katika maisha  na utume wa kimissionari, kwa kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, kwa kujikita katika lugha ya matumaini inayowagusa wengi, hususan vijana mbali kabisa na mambo yanayoweza kuwachefua vijana katika maisha yao.

Huu ni mchakato wa Uinjilishaji unaolenga kuwamegea watu watu tunu msingi za maisha na kweli za kiimani. Hapa Kanisa linaweza kushirikiana na wataalam katika masuala ya mawasiliano ya kijamii ili kusaidia juhudi hizi kwa kutambua matatizo na changamoto zinazoendelea kuzikabili familia mbali mbali duniani. Watambue pia uwepo wa dini na tamaduni, ili kuwa na uwiano mzuri katika mchakato wa ujenzi wa umoja katika tofauti.

Kanisa halina budi kuendelea kuwa macho dhidi ya sera na tamaduni zinazotaka kupandikiza mitindo ya maisha ya ndoa na familia kinyume cha Mapokeo ya Kanisa kama inavyojionesha katika masuala ya kijinsia. Hapa kuna haja ya kutoa malezi na majiundo makini ili waamini na walezi waweze kuwa na dhamiri nyofu wakati wanapotoa maamuzi yao.

Familia za Kikristo hazina budi kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali pamoja na taasisi mbali mbali kwa kutoa mwelekeo na sera sahihi katika masuala ya ndoa na familia. Kwa namna ya pekee, kuna haja ya kuendelea kuhimiza utume wa familia unaokwenda sanjari na utume wa vijana, katekesi na vyama vya kitume, ili kuwawezesha waamini kupata majiundo timilifu katika kila hatua ya maisha.

Hati hii inaendelea kupembua utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa, kama muungano unaoambata uaminifu na upendo wa dhati kati ya bwana na bibi. Kwa wale waliofunga ndoa za serikali wanaweza kusaidiwa taratibu kufikia utimilifu wa mapendo yao kwa kufunga ndoa Kanisani, kama kielelezo cha zawadi inayoimarisha maisha ya wanandoa. Hapa wanandoa wanapaswa kujenga na kuimarisha msamaha, nguzo kuu ya maisha ya ndoa, pale uaminifu ndani ya ndoa unapokosekana, basi, wawe wepesi kurekebisha kasoro hizi, ili kudumisha mahusiano yao.

Kuna haja ya kuwa na mikakati makini na jasiri ili kusaidia ndoa ambazo zina madonda makubwa, kwa kuzionesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kwa wale wanaoishi uchumba sugu, wasaidiwe kuanza mchakato unaowaelekeza katika ndoa ya kudumu, kwa kuwasaidia kutekeleza dhamana hii inayojikita katika huruma na upendo wa Mungu, daima hekima ikipewa kipaumbele cha pekee. Kuanguka na kuvunjika kwa tunu msingi za maisha ya ndoa ni kosa la wote na kwamba, wote wanahaki ya kukimbilia huruma ya Mungu, hasa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao.

Baadhi ya waamini wanaliomba Kanisa kuonesha moyo wa huruma kwa wale ambao wameathirika kutoka na ndoa zao kuvunjika. Hati hii inawataka viongozi wa Kanisa kuwa na maandalizi makini ili waweze kuzifariji ndoa zinazochechemea. Kanisa liwasaidie pia waamini ambao wamebaki kuwa waaminifu katika ahadi zao kwa kutokufunga tena ndoa, ili kuendelea kuonesha uaminifu wao.

Hati ya kutendea kazi inaangalia pia tatizo kuu ambalo lilibanishwa na Mababa wa Sinodi katika Hati yao elekezi mara baada ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia, Kanisa kutoa huduma ya kutengua ndoa bila malipo pamoja na kuepuka hukumu kutolewa mara mbili. Dhana ya mchakato wa kutengua ndoa unaosimamiwa na Askofu mahalia, haukuungwa mkono sana. Hapa waamini wengi wamelitaka Kanisa kuwapatia viongozi wa Mahakama ya Kanisa kutekeleza wajibu wao; kwa kuwa na Mahakama zinazohudumiwa na watu wenye sifa na vigezo.

Hati inawataka Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, Kanisa linaibuka na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zitakazotumiwa kuwashirikisha waamini wote na kwamba, asiwepo mwamini anayesikia kwamba, anatengwa katika maisha na utume wa Kanisa katika maisha ya kiliturujia kwa kujikita katika masuala ya majiundo na mapendo, kwani hata kama ndoa zao zimevunjika, lakini bado ni waamini. Utekelezaji wa mikakati hii ufanywe kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri za watu husika.

Kuhusiana na wanandoa waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena, hati hii inaonesha uwezekano wa mchakato huu kuanza kwa njia ya toba, kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza mchakato huu, chini ya usimamizi wa Askofu maalum. Ni mchakato unaopaswa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kufanya upembuzi wa kina kuhusu chanzo na sababu zilizopelekea kuvunjika kwa ndoa husika pamoja na kuwa na uamuzi wa kujikatalia.

Baadhi ya waamini wanasema, huu ni mchakato unaotafuta ukweli na mwelekeo mpya wa maisha ya kiroho, ili mhusika aweze kusaidiwa na Padre kwa kutambua kwamba, umoja wa maisha ya kiroho unaambata wongofu wa ndani, hali ya neema na umoja wa Kisakramenti.

Hati ya kutendea kazi inaangalia pia ndoa za mseto kwa kutambua kwamba, hili ni tatizo nyeti na kwa sasa halina majibu mepesi, bali kuna haja ya kutengeneza kanuni maadili zitakazowasaidia waamini kuishi vyema imani yao na wale waliobatizwa nje ya Kanisa Katoliki kuwa na uwezekano wa kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ndoa za namna hii zinaweza kuwekwa chini ya tatizo lenye hitaji kuu. Kanisa linaendelea kuonesha ndoa kadiri ya Mafundisho ya Kanisa kwa kukazia Sakramenti ya Upatanisho inayowawezesha waamini kuwa na umoja na Kanisa.

Kanisa linapinga ndoa za watu wa jinsia moja, lakini watu wenye mielekeo hii wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa utu wao; wapokelewe kwa kutambua utata uliopo ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Hapa inashauriwa kuwa na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ndoa za watu wa jinsia moja pamoja na familia zao.

Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hapa Injili ya Uhai inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, kama alivyokaza kusema Mwenyeheri Paulo VI. Hati hii inakazia umuhimu wa kuwaasili watoto pamoja na kuendelea kutoa majiundo makini kwa watoto katika ukuaji wao, kwa kutambua tofauti za kijinsia na dhana ya uumbaji inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi; kama sehemu ya mchakato wa majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kuhusu suala la utoaji mimba, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu na utakatifu wa maisha ya mwanadamu na kwamba, hii ni changamoto ya kuwa karibu na watu wanaokabiliwa na matatizo pamoja na changamoto hizi. Wafanyakazi katika sekta ya afya watambue kwamba, wanao wajibu wa kimaadili na kidhamiri wa kutunza zawadi ya maisha ya mwanadamu. Watu wanahaki ya kufa kifo cha kawaida pasi na kutumbukizwa katika Eutanasia au kifo laini. 

Familia ni shule ya kwanza ya tunu msingi za maisha ya imani na utu wema. Wazazi na walezi wanahamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni walimu wa kwanza na mashuhuda wa imani kwa watoto wao; kwa kuwa makini na wawajibikaji katika masuala ya elimu inayotolewa kwa watoto wao shuleni. Mabibi na mababu wanayo dhamana kubwa katika utume wa familia, wajibu wanaoutekeleza kwa moyo na majitoleo makuu, kiasi cha kuwarithisha imani.

Hati ya kutendea kazi inahitimisha kwa kuangalisha kuhusu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, utakayozinduliwa hapo tarehe 8 Desemba 2015 sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakoyoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba, 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu “wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.