2015-06-22 16:33:00

Wagonjwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, wahudumiwe kwa heshima na upendo


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuzungumza na Familia ya Wasalesiani wa Mtakatifu Yohane Bosco, Jumapili jioni, tarehe 21 Juni 2015, alikwenda moja kwa moja kwenye Kituo cha wagonjwa na walemavu cha Cottolengo. Katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa kuwathamini na kuwahudumia maskini, kwa kuwapatia huduma bora na muhimu katika maisha yao. Kuna maendeleo makubwa ambayo yamekwishapatikana kwenye sayansi na tiba ya mwanadamu pamoja na huduma za kijamii, lakini kwa bahati mbaya, utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu umekuwa na kuanza kuota sugu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, matokeo yake: utu na heshima ya binadamu havipewi tena kipaumbele cha kwanza, bali ulaji wa kupindukia na faida za kiuchumi. Kati ya waathirika wakubwa wa utandawazi na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu ni wazee, ambao idadi yao ni kubwa na wanahudumiwa kwenye kituo cha Cottolengo. Maisha mrefu ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu hayaonekani kuwa ni zawadi na badala yake yanachukuliwa kuwa ni “zigo zito” hususan pale afya inapoyumba miongoni mwa wazee.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mwelekeo huu wa maisha hauna mafao kwa ustawi na maendeleo ya jamii, kumbe kuna haja ya kujenga na kuimarisha mwelekeo mpya unaowaheshimu na kuwathamini wazee na walemavu katika jamii. Kituo cha Cottolengo ni mfano bora wa kuigwa kutokana na upendo unaooneshwa kwa wazee na walemavu wanaohudumiwa katika kituo hiki.

Hapa walimwengu wanaweza kujifunza kuwa na mwelekeo tofauti wa maisha na utu wa binadamu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Giuseppe Benedetto Cottelengo namna ya kumwilisha upendo wa Kiinjili, ili maskini na wagonjwa wengi waweze kupata “nyumba” ya kuishi kama familia, kwa kujisikia kuwa ni sehemu ya jumuiya badala ya kuhisi kwamba, wanatengwa na  kutothaminiwa katika maisha na utu wao kama binadamu.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wagonjwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, kwani wao ni kielelezo cha Mwili wa Kristo ulioteswana kusulubiwa, ambao waamini wanayo heshima kubwa ya kuugusa na kuhudumia kwa wema na upendo mkuu. Cottelengo ni kielelezo makini cha uwepo wa Injili ya upendo wa Kristo inayomwilishwa katika huduma makini.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo nguvu inayowasukuma na kuwachangamotisha watu kusonga mbele kwa imani na matumaini. Yesu alionesha upendeleo wa pekee kwa wagonjwa na maskini. Karama ya Mtakatifu Giuseppe Benedetto Cottolengo imemwilishwa na inaendelea kuzaa matunda yanayojionesha kwa namna ya pekee, miongoni mwa Wenyeheri: Padre Francesco Plaeari na Bruda Luigi Bordino, bila kumsahau Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Carola Cecchini, mmissionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.