2015-06-22 16:02:00

Papa aomba msamaha kwa niaba ya Kanisa Katoliki kwa Wavaldese!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Torino, Jumatatu asubuhi, tarehe 22 Juni 2015 ametembelea Hekalu la Wavaldese lililoko Torino, akasali na kuzungumza na viongozi pamoja na waamini wa Kanisa hili. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Jumuiya ya Wavaldese amegusia kwa namna ya pekee kumbu kumbu ya mahusiano mema iliyobaki moyoni mwake kutoka kwa Waamini wa Kanisa la Wavaldese kule Rio della Plata. Huko alipata nafasi ya kuonja tasaufi, imani na mambo mazuri katika maisha.

Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi cha miaka hamsini ya majadiliano ya kiekumene, kumekuwepo na mfanikio makubwa, kwa kugundua na kuthamini udugu unaofumbatwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake; imani inayowaunganisha Wakristo wote waliobatizwa kwa jina la Yesu. Hiki ndicho kiungo muhimu licha ya tofauti na makando kando yanayoendelea kuwagawa.

Huu ni umoja endelevu ambao bado haujafikia hatima yake. Ni safari ya kiekumene inayojikita katika sala, toba na wongofu wa ndani pamoja na msaada unaotolewa na wanataalimungu sanjari na kazi ya Roho Mtakatifu, kuna matumaini kwamba, iko siku Kanisa litakuwa na umoja unaoonekana na kufumbatwa katika ukweli na upendo.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, umoja miongoni mwa Wakristo ni kazi ya Roho Mtakatifu, ambayo haimaanishi kuwa mambo yote sawasawa. Watu wa asili moja wanaweza kukusanyika kwa pamoja, lakini bado wakaendelea kuonesha tofauti zao msingi. Inasikitisha kuona kwamba, katika historia, tofauti kati ya watu hazikukubalika na kupokelewa kwa mikono miwili na matokeo yake zikawa ni sababu ya kinzani, mipasuko na hata mauaji katika historia ya maisha ya mwanadamu. Ni vitendo ambavyo vimefanywa kwa misingi ya kiimani.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuomba rasmi msamaha kwa niaba ya Kanisa Katoliki, kwa mambo waliyotendewa kinyume cha Ukristo na ubinadamu wao. Lakini leo hii, mahusiano kati ya Makanisa haya mawili yanaendelea kuboreka zaidi na zaidi, kwa kufumbatwa na heshima pamoja upendo wa kidugu, kama inavyojidhihirisha kwa kuwa na Tafsiri ya Biblia inayoyashirikisha Makanisa yote; Nia ya kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa kwa pamoja pamoja na matamko mbali mbali yaliyotolewa na viongozi wa Kanisa kuhusu nyanyaso na dhuluma zinazofanywa dhidi ya wanawake pamoja na mambo mengine msingi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hatua mbali mbali ambazo zimekwishafikiwa hadi sasa ni hamasa ya kusonga mbele katika hija hii ya pamoja, kwa kuonesha umuhimu wa kushirikiana kati ya Kanisa Katoliki la Kanisa la Wavaldese, hususan katika dhamana ya Uinjilishaji; huduma kwa maskini na wote wanaoteseka, hasa maskini na wahamiaji. Tofauti zinazoendelea kuwepo kati ya Wakatoliki na Wavaldese katika masuala mbali mbali zisiwe ni kikwazo cha ushirikiano katika masuala mbali mbali. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha kwa kuwataka Wakristo kutembea kwa pamoja na kwamba, Mwenyezi Mungu atawasaidia kuishi katika umoja unaovuka kinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.