2015-06-22 15:30:00

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu: Kanisa ni chombo cha huruma!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Radio Vatican inakukaribisha tuendelee kuuelewa waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Fransisko Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, itakatozinduliwa hivi karibuni. Katika mfululizo wa vipindi vyetu tunautakafakari wakaraka huu kipengele kwa kipengele, ili ujumbe wake uzame katika akili na mioyo yetu, ili hapo tutakapokuwa tunauadhimisha mwaka huo mtakatifu, sote tujichotee neema tele tunazoletewa na Mama Kanisa.

Katika kipindi kilichopita, Baba Mtakatifu alihitimisha kwa kusisikizia umuhimu wa Kanisa kurudi kwenye misingi, na alikaza kusema “Kanisa litaishi uhalisia wa maisha yake endapo tu litaungama na kutangaza huruma na msamaha”, kitu ambacho ndiyo hulka haswa ya Mungu muumbaji na Mwana Mkombozi. Kwa kufanya hivyo Kanisa litawaleta watu wengi zaidi karibu na Chemchemi ya Huruma, ambaye ni Kristo Mwenyewe.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema ndani ya Misericordiae vultus, Kanisa limedhaminishwa kutangaza huruma ya Mungu,  ambayo ndio mdundo wa moyo wa Injili ambayo kwa namna yake ni lazima izame katika mioyo na mawazo ya kila mtu. Mchumba wa Kristo (yaani Kanisa) lazima ajiunde hivi ili tabia zake zirandane na zile za Mwana wa Mungu aliyetoka na kujitoa kwenda kwa kila mtu bila ubaguzi.

Katika siku zetu hizi ambapo Kanisa linajikita katika shughuli  ya uinjilishaji mpya, tema ya huruma inahitaji kukumbushwa tena na tena, kwa ari mpya na katika mtindo mpya wa Kichungaji. Huruma ni muhimu sana kwa Kanisa na kwa ajili ya unadhifu wa ujumbe ambao Kanisa lenyewe linaufundisha, linauishi na kuushuhudia. Lugha yake na matendo yake lazima vioneshe huruma ili kuweza kugusa mioyo ya watu wote na kuwaangazia ili waweze kuona njia iwapelekayo kwa Baba.

Ukweli msingi kabisa wa Kanisa ni upendo kwa Kristo. Kanisa lazima lijifanye lenyewe kuwa ni mtumishi wa upendo huo na liupeleke kwa watu wote; upendo ambao husamehe na hujionesha zaidi katika kujitoa kwake. Hatimaye, kwa vyovyote vile ambavyo Kanisa lipo, upendo wa Baba hudhihirika. Katika Parokia zetu, katika jumuia zetu, katika vyama mbalimbali vya kitume na vikundi vya sala: kwa kifupi popote pale walipo Wakristo, kila mmoja lazima aonje chemchemi ya huruma; anasema Baba Mtakatifu.

Ni mwaliko wa Baba Mtakatifu kuimwilisha na kuiishi huruma ya Mungu ili kweli sisi tuaminio katika jina la Kristo tuonekane kwa namna yetu ya kuishi. Huwa inakuwa bahati mbaya kubwa pale ambapo wale tunaolitaja jina la Kristo na kuitwa Wakrito, japo tunapenda kuhurumiwa na kusamehewa, sisi wenyewe tunakwepa kuwa na huruma na kuonesha huruma kwa wenzetu.  Si mara chache, kwa sababu ya kukosa huruma ndani ya Kanisa, tunaendekeza malumbano yasiyo na msingi na yasiyokoma. Ndipo hapo tutakuta vyama vya kitume vinachambuana na kushushana thamani, vikundi vya sala vinadharauliana na kularuana, kila mmoja akitaka kuwa bora zaidi kuliko mwenzake. Katika mantiki hiyo Baba Mtakatifu anasema hatuidhihirishi huruma ya Mungu, bali tunajitafuta na kujitukuza sisi wenyewe.

Mbinu za kuidhihirisha huruma ya Mungu ni pamoja na kuwa tayari kujifahamu na kujipokea; halafu kuwa tayari kuwafahamu wengine jinsi walivyo na kuwapokea kama walivyo, ni hivyo tu tutaweza kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Jitihada zetu za kuimwilisha huruma ya Mungu zinahujumiwa na tabia yetu ya kutaka wangine wote wafikiri kama sisi, waongee kama sisi, watende kama sisi, watamani tunayotamani sisi, wayaseme tunayotaka kuyasikia sisi au waishi kama sisi. Kama wakiwa kinyume nasi, basi hao hawafai na ni maadui zetu!! Hasha, maisha ya safari ya imani siyo hivyo!

Maisha ya imani yanahitaji sadaka sana. Na sadaka mmoja wapo ni kuwapokea wale ambao wanafikiri, kutenda na na kuishi kinyume nasi. Hapa mpendwa msikilizaji mwaliko ni kwamba: tuwape na wengine nafasi ya kuwa wao. Ila sisi kama tunaomwamini Kristo, imani yetu inayomwilishika katika matendo mema ya upendo na huruma ndivyo viwafanye hao wenzetu, waitambue huruma ya Mungu tunayoisadiki, kuifundisha na kuiishi, na wakitaka watatufuata kutokana na mwenendo wetu mwema wa maisha ya kiimani na kijamii.

Tunalirudia kwa hekima neno lile: huruma na upendo wa Mungu si swala la maneno-maneno, bali ni matendo halisi katika maisha. Mwito wa pekee kwa mwaka huu mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kuitambua zaidi huruma ya Mungu, kuipenda zaidi huruma ya Mungu, kuishukuru zaidi huruma ya Mungu, kuimwilisha zaidi huruma ya Mungu na kuitangaza zaidi huruma hiyo ya Mungu kwa maneno na matendo ya maishani.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican tunakushukuru kwa kuitegea sikio Radio ya Kanisa Katoliki. Kwa roho ya upendo na huruma inayoinua, msisitize na mwenzako asikose kuisikiliza Radio Vatican. Katika mwezi huu tuendelee kusali kuomba huruma ya Yesu tukisema: Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako amina.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.