2015-06-22 15:41:00

Baba Mtakatifu Francisko afunika Torino! Ziara imegusa maisha ya wengi!


Padre Ciro Benedettini, msemaji mkuu msaidizi  wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameridhishwa na kufurahishwa sana na mapokezi makubwa yaliyofanywa na Familia ya Muungu Jimbo kuu la Torino wakati wa hija yake ya kichungaji ya siku mbili, kuanzia tarehe 21 hadi 22 Juni 2015. Kila tukio limekuwa na uzito na maana ya pekee.

Kwa kukutana na kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi na wafanyabiashara; kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Vittorio, ambako umeshuhudia bahari ya watu ikiwa imefurika ili kushiriki katika Mafumbo ya Kanisa. Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kukutana na kuzungumza na Familia ya Wasalesiani wa Don Bosco; kwa kusali mbele ya Sanda Takatifu; kwa kukutana na kuzungumza na vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia pamoja na kuzungumza na waamini wa Kanisa la Wavaldese huko Torino.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa anasema, hija yake kwenye Kanisa la Mtakatifu Theresa, ambalo kunako mwaka 1907 Babu na Bibi yake wanaojulikana kama Giovanni Bergoglio na Rosa Vassallo walifunga pingu za maisha na kunako mwaka 1908, Baba yake mzazi Mario akapewa Sakramenti ya Ubatizo, ni tukio ambalo limeipamba hija hii kwa namna ya pekee, kwa kumrudisha tena katika historia kwa kutambua na kukazia umuhimu wa familia.

Katika Kanisa la Mtakatifu Theresa, Papa amesali kwa ajili ya kuziombea familia mbali mbali pamoja na kuomba mafanikio mema wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican, kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba, 2015. Padre Ciro Benedettini anabainisha kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Torino, imekuwa ni safari ya kurejea tena katika asili yake.

Itakumbukwa kwamba, alipokuwa nchini Argentina, mara kwa mara alikuwa anakuja nchini Italia, kutembelea maeneo walimo toka wazazi wake. Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na ndugu na jamaa zake wa karibu. Wakati wa mchana, wameshiriki pamoja chakula cha mchana Uaskofuni. Hafla hii imehudhuriwa na watu 30. Inapendeza kwa kweli, kuona ndugu wakiishi kwa umoja na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.