2015-06-21 11:06:00

Mwaka wa Watawa Duniani iwe ni fursa ya kuambata: Karama, Mashauri na Ushuhuda


Askofu Patrick Chisanga wa Jimbo Katoliki Mansa, nchini Zambia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, ni tukio la furaha, neema na baraka; ni changamoto na mwaliko kwa watawa kuendelea kujisadaka zaidi na zaidi kwa ajili ya Mungu na jirani zao, kwa kutambua kwamba, Mama Kanisa anawatambua na kuwathamini katika maisha na utume wao; katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaowasukuma kuwahudumiwa Watu wa Mungu kiroho na kimwili.

Mwaka wa Watawa Duniani unakwenda sanjari na Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Upendo Mkamilifu, Perfectae caritatis, inayowataka watawa kufanya mageuzi makubwa katika maisha yao kwa kujikita katika karama za waanzilishi wa mashirika, nadhiri, maisha ya kijumuiya yanayofumbatwa katika maisha ya sala.

Askofu Chisanga anasema, Mwaka wa Watawa Duniani, iwe ni fursa kwa watawa kufanya tafakari ya kina kuhusu: karama na utume wao katika Makanisa mahalia; umuhimu wa maisha ya kijumuiya kama ushuhuda wa kinabii; wajiulize wapi ambapo wameonekana kupata mafanikio makubwa katika maisha na utume wao; wachunguze ni wapi ambao wameshindwa  na kuanguka, ili kufanya toba na kukimbilia huruma ya Mungu, tayari kuanza tena upya, kwa imani na matumaini.

Askofu Patrick Chisanga anakumbusha kwamba, watawa ni watu walioteuliwa kutoka ndani ya familia kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Kumbe, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa ni mwaliko kwa waamini walei kushiriki kikamilifu katika kuwaombea na kuwasindikiza watawa katika maisha na utume wao, huku wakiwasaidia kwa hali na mali.

Watawa wanapaswa kushirikiana na familia ili kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Watawa na waamini walei, washirikiana kwa dhati kabisa katika kutangaza Injili ya Familia, kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaojikita katika tunu msingi za maisha ya kifamilia na kijumuiya.

Askofu Chisanga anasema, Watawa wamekuwa na mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Zambia, kiasi kwamba wameacha chapa ya kimissionari katika maisha ya Familia ya Mungu nchini humo. Kuanzishwa, kukua na kuendelea kwa Kanisa Katoliki nchini Zambia ni matunda ya jasho la Wamissionari watawa waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inaenea sehemu mbali mbali za dunia.

Zambia inaendelea kuwashukuru na kuwapongeza watawa wa Mashirika mbali mbali kutokana na huduma makini wanayoitoa katika sekta ya elimu, afya, mawasiliano na maendeleo kwa ujumla. Watawa ni utajiri mkubwa wa Kanisa nchini Zambia na Afrika kwa ujumla. Pamoja na mchango wote huu, lakini watawa wanapaswa daima kujitajirisha zaidi na zaidi katika maisha yao ya kiroho kwa kujikita katika: Sala, Tafakari na Maisha ya Kisakramenti, ili kupata nguvu ya kuwahudumia Watu wa Mungu kwa upendo mkuu na huruma, kwa kutambua na kuheshimu utu wao kama binadamu.

Askofu Chisanga anasema, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unachangamoto na matatizo yake, jambo la msingi kwa watawa ni kuhakikisha kwamba, kamwe hawamezwi na kutumbukizwa katika malimwengu kwa kuelemewa na uchu wa mali na madaraka; kwa kukandamizwa na upweke hasi, kiasi cha kupata kishawishi cha kutafuta faraja nje maisha ya kitawa na matokeo yake, huko watakiona cha mtema kuni!

Askofu Patrick Chisanga anasema, kwa miaka mingi Kanisa Barani Afrika lilitegemea misaada mingi kutoka Ulaya na Marekani, lakini sasa umefika wakati kwa Kanisa kuanza mchakato wa kujitegemea kwa rasilimali watu, fedha na vifaa. Ni wakati wa kuhakikisha kwamba, hata Mashirika ya kitawa yanajiwekea mikakati ya kuweza kujitegemea kwa kujikita katika kanuni maadili, ukweli na uwazi, vinginevyo, watakumbana na wajanja wachache watakaowaliza kwa kuwakwapulia hata kile kidogo walicho nacho kwa ajili ya maskini!

Kuna kishawishi kikubwa kwa watawa kumezwa na malimwengu, kumbe, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, ile ni fursa ya kujikita katika Mashauri ya Kiinjili na Maisha ya Kijumuiya, ili kuonesha ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa wawaonjeshe walimwengu, furaha, matumaini na ushuhuda wa kinabii kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.