2015-06-21 11:23:00

Chanzo kikuu cha umaskini wa kimaadili na kiutu ni uchu wa mali na madaraka!


Familia ya Watu wa Mungu nchini Hispania inaendelea kuonja athari za myumbo wa uchumi kimataifa unaojionesha kwa namna ya pekee katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kimaadili. Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaonesha ushuhuda wa imani, upendo na mshikamano na wale wote wanaoteseka na kuogelea katika shida na mahangaiko ya kiroho, kimwili na kimaadili. Ikumbukwe kwamba, Kanisa linatumwa kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu katika mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.

Huu ni Waraka wa kichungaji ulioidhinishwa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika mkutano wao, baada ya kupembua kwa kina na mapana madhara ya myumbo wa uchumi kimataifa na kwamba, Kanisa linatambua dhamana yake ya kuwahudumia Watu wa Mungu, ili waweze kuwa na imani na matumaini ya kuweza kusonge mbele licha ya magumu na kinzani nyingi wanazokabilia nazo katika maisha.

Waraka huu umegawanyika katika sehemu kuu nne: Unaanza kwa kupembua hali halisi ya maisha ya kijamii nchini Hispania: matatizo, fursa na changamoto zilizopo na ambazo zinaweza kufanyiwa kazi kwani ni mambo yanayopata asili yake kutoka nchini Hispania. Kuna idadi kubwa ya watu wanaotumbukia katika umaskini wa hali na kipato kila siku ya maisha yao na kwamba, familia nyingi zimeathirika vibaya sana kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa, kiasi kwamba, hata leo hii zinashindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.

Maaskofu wanabainisha kwamba, kuna kundi kubwa la vijana ambalo halina fursa ya ajira, kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha yaliyo bora leo na kesho. Umaskini mwingine ni ule ambao unafumbatwa katika changamoto ya wahamiaji, ambao wanateseka kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linaiomba Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya pamoja na Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba, wanawahudumia wakimbizi na wahamiaji sanjari na kushirikiana na nchi wanamotoka.

Umaskini mpya unaendelea kushika kasi katika masuala ya kijamii na kisiasa kwa kukumbatia rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Maaskofu wanasema, huu ni umaskini wa kimaadili na kiutu. Chanzo cha umaskini huu ni uchu wa mali, utajiri na madaraka na matokeo yake ni Serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake barabara kwani fedha ya umma inaishia mikononi mwa watu wachache na familia zao. Maaskofu wanawaalika wananchi wa Hispania, kuwa na mwelekeo mpya wa maisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: ustawi na mafao ya wengi; kwa kuimarisha kanuni maadili na utu wema sanjari na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo kwa jirani.

Umaskini mpya unajionesha hata katika maisha ya kiroho, kiasi kwamba, watu wanataka kumgeuzia Mungu kisogo na kumwondoa kabisa katika sera na mikakati ya maisha yao; matokeo yake ni kudhalilisha utu na maisha ya binadamu pamoja na haki zake msingi. Ikumbukwe kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, nje ya Mwenyezi Mungu, utu na heshima ya binadamu viko hatarini. Mwenyezi Mungu ni kiini rejea katika maisha ya kiutu na kimaadili, chanzo cha upendo na mshikamano wa kidugu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linabainisha kwamba, matatizo mengi yanayoendelea kuwakumba wanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni tabia ya kutojali utu na heshima ya binadamu. Watu wanamezwa mno na malimwengu pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwamba, uchumi unakuwa ni chanzo kikuu cha myumbo wa tunu msingi katika maisha ya watu wengi.

Hapa watu wengi wanajikuta wakiogelea kwenye dimbwi la madeni kiasi hata cha kushindwa kulipia pango la nyumba. Baadhi ya wachumi na watunga sera wamekuwa wakijikita katika mchakato wa kutafuta faida kubwa na matokeo yake ni mateso na mahangaiko ya watu wengi. Sera za ukuaji wa shughuli za kiuchumi na utoaji wa huduma, zinaendelea kuwa ni chanzo cha manung’uniko, migomo na kinzani za kijamii.

Ikumbukwe kwamba, uchumi si kigezo peke yake kinachoweza kuboresha maisha ya watu katika medani mbali mbali. Hapa wanasiasa wanahamasishwa kwa namna ya pekee kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi na kwamba, huu ni wajibu wao msingi. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linakaza kusema kwamba, Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, hawana budi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika huduma ya mapendo na uchumi unaojali na kushirikisha wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.