2015-06-20 14:43:00

Ukosefu wa fursa za ajira ni janga la kijamii, binadamu apewe kipaumbele!


Shirikisho la Kitaifa la wafanyakazi mashuhuri nchini Italia kwa takribani miaka mia moja, limechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji  wa masuala ya biashara na uchumi, kiasi cha kutengeneza fursa za ajira pamoja na kukuza soko la kimataifa la bidhaa zinazozalishwa nchini Italia.

Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi mashuhuri kiasi cha kuwapatia tuzo maalum, changamoto ya kuendelea kujifunga kibwebwe ili kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, ambao unaendelea kuwatendea watu wengi ndani ya jamii, kwa kusababisha mpasuko wa kijamii na waathirika wakubwa ni vijana.

Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana ni janga la kijamii, kwani vijana ni sehemu muhimu sana ya nguvu kazi katika masuala ya kiuchumi, kwani vijana bado damu inachemka sana. Vijana wanapaswa kusaidiwa ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao katika ulimwengu wa kazi, lakini kwa bahati mbaya, hali inaonesha kwamba, kwa sasa vijana hawana nafasi tena katika mchakato wa uzalishaji na utoaji huduma. Huu ni mwelekeo potofu wa kitaifa na kimataifa.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 20 Juni 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Kitaifa la wafanyakazi mashuhuri nchini Italia. Baba Mtakatifu anasema kwamba, mafao ya wengi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa hayana budi kuwahusisha watu wote wanaounda jamii husika kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kama kiini na lengo la maendeleo endelevu. Jamii nzima isipohusishwa kikamilifu, kuna hatari ya kutofikiwa kwa mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwani wamethubutu, wameonja hatari, lakini hawakukata tamaa wakasonga mbele kwa kuwekeza katika mawazo, nguvu na mitaji, ili kuzalisha kwa kugawanya majukumu; kutafuta na kushirikisha matokeo; pamoja na kuwahamasisha wengine ili kushirikiana zaidi. Huu ndio mlango wa kazi za kijamii; unaowashirikisha wengi na kugawanya majukumu; ili kuhamasisha hali ya kutegemeana; ugunduzi na uwajibikaji wa pamoja. Mambo haya yana mwelekeo chanya kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuwa na matumaini na fursa mbali mbali kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu analipongeza Shirikisho hili kwa kukazia si tu kwa kuchangia katika masuala ya kijamii, bali pia wanachama wake wahakikishe kwamba, wanajikita katika kanuni maadili, ili haki na utawala wa sheria viweze kushika mkondo wake katika masuala ya uchumi na maendeleo ya watu. Hii ni changamoto ya kuwa mbali na vitendo vya rushwa na ufisadi, ili kweli haki inayoambata usawa, sheria, dhamiri nyofu na kwa ajili ya mafao ya wengi iweze kutawala.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, mtu mwenye haki, atajitaabisha kuwajali na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kuibua njia mpya zinazoweza kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. Wanachama wa Shirikisho la kitaifa la wafanyakazi mashuhuri liko chini ya usimamizi na ulinzi wa Mtakatifu Benedikto wa Norcia. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuwakabidhi kwa Mtakatifu Benedikto wa Norcia pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.