2015-06-20 16:50:00

Ukarimu na msaada kwa wakimbizi na wahamiaji ni dhamana ya kimaadili


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye Makao yake makuu mjini Geneva, hivi karibuni wakati akichangia mada kuhusu haki msingi za wahamiaji kwenye mkutano wa Baraza la Haki za binadamu anasema kwamba, nchi za Ulaya zinapaswa kufungua mipaka yake ili kuwahudumia wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya maisha na kisiasa. Jumuiya ya Kimataifa iwe ni mwelekeo sahihi na mbinu mkakati wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kutambua haki zao msingi.

Wakimbizi na wahamiaji wapewe hifadhi katika mazingira yanayostahili hadhi na heshima ya binadamu na kwamba, vyombo vya habari visaidie kutangaza ukweli na wala si kuchochea chuki na uhasama kati ya watu. Wapewe hifadhi na kuthaminiwa kama binadamu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anakaza kusema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haijafanikiwa kuwahudumiwa kikamilifu wakimbizi na wahamiaji na matokeo yake, wengi wao wanakufa maji baharini au kwa njaa na kiu huko jangwani. Kuna idadi kubwa ya watoto kwenye makundi ya wahamiaji, ambao hawana msaada kutoka kwa wazazi wao, idadi hii inatisha sana. Kutokana na changamoto zote hizi, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuhakikisha kwamba, wahamiaji na wakimbizi wanahudumiwa kwa ukamilifu.

Ikumbukwe kwamba, wahamiaji ni rasilimali na nguvu kazi inayoweza kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu, kumbe, suala ya wakimbizi na wahamiaji halina budi kuangaliwa: kisiasa, kidini, kiuchumi na kijamii. Ili kufanikisha lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu badala ya kujenga kuta za utengano na ubaguzi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.

Inasikitisha kuona kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanatelekezwa katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu. Kuwapokea na kuwakirimia wahamiaji na wakimbizi ni dhamana ya wote pasi na ubaguzi pamoja na kuhakikisha kwamba, haki zao msingi zinalindwa na kuthaminiwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.