2015-06-20 15:25:00

Ujumbe kwa waamini wa dini ya Kiislam wakati wa Siku kuu ya Id Al Fitri


Mwezi mkutufu wa Ramadhani kwa waamini wa dini ya Kiislam ni kipindi cha swala, kufunga na kutoa sadaka pamoja na kuwasaidia maskini. Ni wakati wa kutembelea ndugu, jamaa na marafiki. Kama ilivyo desturi, Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, limewatumia waamini wa dini ya Kiislam, ujumbe kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya  Id al Fitri 1436h/ 2015 A.D.

Baraza la Kipapa linawatakia waamini wote wa dini ya Kiislam baraka, amani na utulivu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Id al Fitri. Ni matumaini ya Baraza la Kipapa kwamba, matunda ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani yatasaidia kuyatajirisha maisha yao ya kiroho. Lakini katika kumbu kumbu hii, kuna watu ambao wamewapoteza ndugu na jamaa zao; wengine wanaendelea kuteseka na kuhangaika: kiroho na kimwili kutokana na vurugu.

Kuna makundi makubwa ya makabila na waamini wa dini mbali mbali ambao wameathirika kutokana na ukosefu wa haki; baadhi yao wameuwawa kikatili; urithi na utajiri wa kidini na kitamaduni vimesambaratishwa; wanawake na wasichana wamenyanyaswa kijinsia na baadhi yao kugeuzwa kuwa ni watumwa wa ngono. Kuna makundi makubwa ya watu ambayo yametekwa nyara na kuuzwa kwenye soko haramu la biashara ya binadamu; wengine viungo vyao vimechomolewa ili kuuzwa. Inasikitisha kuona kwamba, hata maiti pia zimeuzwa.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini linasema kwamba, watu wanatambua madhara ya uhalifu huu, lakini mbaya zaidi ni vitendo vya kihalifu vinavyohalilishwa kwa jina la dini. Huu ni ushuhuda kwamba,  kuna baadhi ya watu wanaotaka kutumia dini kwa mafao yao binafsi, ili kujipatia utajiri na madaraka. Ikumbukwe kwamba, viongozi wenye dhamana ya kulinda watu na mali zao, wanawajibika pia kuwakinga dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kwa upande mwingine, kuna watu ambao wanadhama ya kutoa elimu: hizi ni familia, shule, vitabu vya shule, viongozi wa kidini pamoja na mahubiri na hotuba zao mbali mbali  bila kusahau vyombo vya habari. Dhana ya uhalifu na vitendo vya kigaidi, kwanza kabisa inachipuka kutoka kwenye akili ya binadamu ambaye amepotea na hatimaye, kutekelezwa katika uhalisia wa maisha ya binadamu.

Wadau mbali mbali wenye dhamana ya kutoa elimu kwa vijana wa kizazi kipya hawana budi kuhakikisha kwamba, wanawafundisha umuhimu wa kuthamini na kutunza zawadi ya uhai, utu na heshima ya kila binadamu bila kujali: kabila, dini, tamaduni, tabaka au chama chake cha kisiasa. Kwani hakuna mtu ambaye ana haki ya kuua kwani kwa kufanya hivi ni kwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu na dhidi ya mwanadamu mwenyewe.

Mchakato wa elimu hauna budi kuwa makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu na jamii husika, kwa kujikita katika ukweli na mafao ya wengi. Wakristo na Waislam kwa pamoja wanamwangalia Mwenyezi Mungu kama kiini cha mahusiano yao na chemchemi ya ukweli. Huu ndio mwelekeo sahihi unaopaswa kufuatwa na waamini wa dini mbali mbali kwa kujenga mahusiano mema na Mungu pamoja na jirani zao.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo wana nafasi ya kusali na kwamba, watu wana kiu ya sala kwa ajili ya: kujenga na kudumisha: haki, amani na usalama duniani; kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; ili wale waliokengeuka waweze kumrudia tena Mwenyezi Mungu kwa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yao. Ili hatimaye, waweze kujisadaka kwa ajili ya maskini na wagonjwa.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika ujumbe wa Siku kuu ya Id Al Fitri linasema kwamba, sherehe za kidini miongoni mwa waamini zinaleta matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Haya yawe ndiyo matamanio ya waamini wengi katika uhalisia wa mambo. Kwa kuungana na Baba Mtakatifu Francisko, Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, linawatakia mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hatimaye, amani, furaha na ustawi katika maisha ya waamini wa dini ya Kiislam sanjari na makuzi yao kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.