2015-06-20 17:11:00

Simameni kidete kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa, familia na malezi!


Askofu mkuu Vincenzo Pagilia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia katika ujumbe wake kwa kamati ya kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia nchini Italia, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema,  kusimama kidete kulinda na kuwatetea watoto dhidi mafundisho potofu yanayotaka kukazia masuala ya kijinsia kinyume cha mapokeo, tamaduni, utu na heshima ya binadamu.

Waamini kutoka Jimbo kuu la Roma pamoja na watu wenye mapenzi mema, Jumamosi, tarehe 20 Juni 2015 wanafanya maandamano makubwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, ili kupinga sera zinazotaka kuhalalisha masuala ya kijinsia kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Askofu mkuu Paglia anataka waamini watambue kwamba, familia ni kiini cha maisha ya kijamii, mahali ambapo watu wanajifunza kuthamini tofauti zinazojitokeza na kwamba, wazazi na walezi wanakuwa na dhamana ya kurithisha imani na tunu msingi kwa watoto wao.

Familia ya Kikristo inafumbatwa katika upendo kati ya bwana na bibi, unaoimaarishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa na matunda ya muungano huu, ni watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Familia ni rasilimali inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Familia imekuwa ni nyumba ya maskini, wagonjwa na wazee kwa kutoa hifadhi na huduma makini.

Askofu mkuu Paglia anasema kwamba, Kanisa linatangaza Injili ya huruma na upendo wa Mungu, linawapenda na kuwathamini watu wote, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mama Kanisa anapenda kutangaza na kushuhudia uzuri, wema na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwa kukazia: umoja, upendo na mshikamano, zawadi ya maisha na heshima kwa kila mtu, ili kukumbatia Injili ya Uhai. Tofauti mbali mbali zinazojitokeza ndani ya familia ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe si kikwazo cha kuondolewa.

Watoto wanao haki ya kuzaliwa, kulelewa na kukulia katika mazingira ya familia inayoundwa kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo, kwani huu ndio mpango wa Mungu kwa binadamu. Kanisa linapenda kuwahimiza wakristo kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha familia zinazojikita katika msingi wa Injili na Mfundisho ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, ndani ya moyo wa mwanadamu kuna hamu na kiu ya kutaka kujenga umoja wa familia.

Ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku za usoni unategemea kwa namna ya pekee, jinsi jamii inavyothamini na kuheshimu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Dhamana na wajibu huu unawataka watu kuwajibika barabara pasi na mzaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.