2015-06-20 08:53:00

Jifungeni kibwebwe kupambana na rushwa nchini Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Alhamisi, Juni 18, 2015, amepokea matreka makubwa 10 ambayo yametolewa na Kampuni ya New Holland Agriculture ya India kama zawadi kwa mkulima wa Tanzania. Matreka hayo aina ya TD5.90 yametolewa na Kampuni hiyo baada ya Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete kutembelea kiwanda hicho cha New Holland Agriculture kilichoko katika eneo la Greater Noida, nje kidogo ya Mji wa New Delhi, mji mkuu wa India, ambako Rais Kikwete anafanya ziara rasmi ya siku nne kwa mwaliko wa Rais Pranad Mukherjee.

Kiwanda hicho ambacho huzalisha matrekta ya kisasa kabisa 58,000 kwa mwaka kimekuwa kinafanya biashara na Tanzania tokea mwaka 2011 wakati kilipouza matrekta 700 kwa Shirika la Biashara la Jeshi la Kujenga Taifa la SUMA JKT. Mpaka mwisho wa mwaka huu, imepangwa kuwa shirika hilo la JKT litanunua matrekta mengine 300 kwa ajili ya kuboresha na kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania.

Mbali na kuuza matrekta hayo, New Holland Agriculture ambacho soko lake kuu ni nchi za Ulaya na Marekani pia kimefundisha mafundi mchundo 26 kutoka JKT na walimu wa walimu watano tokea mwaka jana, 2014. Pamoja na kwamba trekta la New Holland lilianza kuzalishwa na Kampuni yake mama ya CNH Industrial mwaka 1895, ilikuwa mwaka 1996 wakati New Holland Agriculture ilipoanzisha kiwanda katika Greater Noida, India. Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa asilimia 100 na CNH Industrial.

Kampuni hiyo ya New Holland Agriculture ni moja ya makampuni ambayo yanaongoza dunia kwa kutengeneza vifaa vya kilimo na hasa matrekta ya kulimia na matrekta makubwa ya kuvunia mazao (harvesters). Kampuni mama ya CNH Industrial ni kampuni kiongozi wa utengenezaji wa vifaa mbali mbali vya viwandani ikiwa inaendesha shughuli zake katika nchi 190 duniani na kutengeneza aina 12 za vifaa katika viwanda 62 na vituo vyake vya utafiti 48, shughuli ambazo kwa pamoja zinaajiri watu 71,000.

Watendaji wakuu makampuni ya India waimwagia sifa Tanzania

Watendaji wakuu wa makampuni makubwa ya India na Wafanyabiashara wengine wa nchi hiyo wameisifia Serikali ya Tanzania na sera zake za kuendeleza viwanda na kuvutia uwekezaji wakieleza utendaji wa Serikali katika eneo hilo kuwa ni wa uwazi mkubwa, wenye urafiki na unaovutia. Aidha, watendaji wakuu hao wamesema kuwa Tanzania ni nchi nzuri kuwekeza kwa sababu ya amani, utulivu na utawala wa kisheria nchini humo.

Watendaji wakuu na wafanyabiashara hao wametoa pongezi hizo Alhamisi, Juni 18, 2015, wakati walipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye yuko katika ziara rasmi ya Kiserikali katika India kwa mwaliko wa Rais Pranad Mukherjee. Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Taj Palace ambako Rais Kikwete ambaye anafuata na Mama Salma Kikwete, ndiko alikofikia, Watendaji wakuu hao, mmoja baada ya mwingine, wamesifia sera za Serikali ya Tanzania kuhusu uwekezaji na urafiki wa watendaji wake kwa wawekezaji.

Mara baada ya Rais Kikwete kutoa hotuba ya kusisimua kuelezea fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Tanzania, Mwakilishi wa Kampuni ya airtel, Bwana Shirshirv Priyadarsh amemwambia Rais Kikwete: “Sisi airtel, tumekuwa katika Tanzania kwa miaka mingi sasa.Tunaamni kuwa kuhusu suala la biashara na uwekezaji, Serikali yako Mheshimiwa Rais inaendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu, pengine kuliko nchi nyingine yote ya Afrika.” “Kuna mambo makubwa matatu, uchumi wa Tanzania na sera zake za uwekezaji unaendeshwa kwa wazi mkubwa, Serikali na sera zake ni za kirafiki kwa uwekezaji na wawekezaji na pia ni sera zinazovutia mwekezaji yoyote kuwekeza katika uchumi huo.”

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Tibabu ya Appolo amesema kuwa kwa sababu ya urahisi wa kufanya biashara katika Tanzania, kampuni hiyo itafungua mjini Dar Es Salaam, kliniki yake ya kwanza katika Tanzania ili kupunguza mzigo wa Watanzania wanaosaka huduma za tiba kulazimika kusafiri hadi India.

“Hatuna shaka kuwa ni rahisi kuwekeza na kuendesha shughuli katika Tanzania na hivyo katika miezi miwili ijayo, tutakuwa tunafungua kliniki yetu ya kwanza katika Tanzania,”amesema mama huyo ambaye alikuwa miongoni mwa watendaji wakuu wa makampuni 30 ya India kuhudhuria mkutano huo na Rais Kikwete.

Naye mwakilishi wa magari ya Kampuni ya Mahindra amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa inaendesha shughuli zake katika Tanzania kwa muda sasa. “Kwa sababu ya kuridhishwa kwetu na sera nzuri za uwekezaji wa Tanzania sasa tunaomba kushirikiana na serikali kujikita kwa nguvu katika utengenezaji matrekta na kufungua viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo katika Tanzania.” Kampuni ya magari ya Tata ambayo imekuwa katika Tanzania kwa miaka 20 sasa imesema kuwa sasa inataka kuanza kutengeneza mabasi katika Tanzania kwa ajili ya masoko ya Kusini mwa Afrika hasa Zimbabwe na Malawi.

JK: Tunazungumzia zaidi rushwa kwa sababu ya hatua za Serikali

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Watanzania wamepata uelewa mkubwa wa rushwa na athari zake kwa sababu Serikali imechukua hatua nyingi za kujenga uwezo wa taasisi ambazo zinakabiliana na rushwa katika Tanzania kwa kiasi kikubwa na pia kuweka misingi thabiti ya kisheria ya kukabiliana na jambo hilo. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kazi ya kukabiliana haiwezi kuwa ya mtu mmoja, ya Rais pekee kwa kutoa maagizo na maelekezo bali kazi hiyo itafanikiwa vizuri zaidi kama kazi hiyo itafanywa na taasisi ambao zinazidi kuongeweza ukweli kila wakati.

Rais Kikwete alizungumzia suala hilo la rushwa usiku wa Jumatano, Juni 17, 2015, wakati alipokutana na kuzungumza na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini India kwenye Hoteli ya Taj Palace, mjini New Delhi, kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake rasmi ya siku nne nchini India kwa mwaliko wa Rais wa India, Mheshimiwa Pranad Mukherjee.

Akijibu maswali mbali mbali ya Watanzania hao, Rais Kikwete alisema: “Kuna mwamko mkubwa zaidi kuhusu vita dhidi ya rushwa kwa sababu Serikali imeongeza sana uwezo wa taasisi zinazoongoza mapambano dhidi ya rushwa.” “Tumeimarisha sana uwezo wa TAKUKURU, tumeongeza sana nguvu ya PPRA, tumepanua uwezo wa Ofisi ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa, tena kwa uwazi, ndani ya Bunge. Haya yote yameongeza uelewa na mwamko wa wananchi kupigana kwa nguvu zaidi na rushwa,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kisheria hivyo hivyo taasisi hizo zimeongezewa nguvu. Hata makosa yenyewe ya ulaji rushwa yameongezwa kisheria kutoka manne ya mwaka 2005 hadi kufikia 24. Hili nalo la sheria limeziongezea taasisi zetu nguvu ya kufanya kazi ya kukabiliana na rushwa. Rushwa sasa inatambuliwa kwa urahisi zaidi kuliko zamani.”

Rais pia amesema kuwa ni makosa ya jinai kuwatoza malipo ya huduma mbali mbali nchini kwa fedha za kigeni na hasa dola. “Kwa wageni sasa, wanakuja na dola zao wakitaka kununua bidhaa mbali mbali nchini. Wao kulipa kwa dola ni barabara.” Aliongeza:“Lakini kwa Watanzania hapana. Hawa wanastahili kulipia huduma mbali mbali kwa sarafu ya Tanzania. Huwezi kumtoza mzazi Mtanzania malipo ya ada ama karo ya mtoto wake katika fedha za kigeni. Lakini kwa mgeni, kwa nini tusimtoze kwa dola?”

Kuhusu ongezeko la ajali nchini, Rais Kikwete alisema kuwa ni kweli ajali zimeongezeka nchini kwa sababu mbali mbali ikiwamo kutokana na ongezeko kubwa la magari katika barabara zetu pamoja na uzembe na ulevi wa madereva. “Mwaka 2005, Tanzania nzima ilikuwa na magari yaliyokadiriwa kufikia milioni 1.72. Lakini katika miaka 10 tu iliyopita, yameongeka magari 1.5 milioni. Hili ni ongezeko kubwa sana pamoja na jitihada zetu za kujenga na kupanua barabara zetu nchini,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Ni kweli tunahitaji kupanua barabara zetu, lakini madereva nao wanachangia sana ajali kwa ulevi na uzembe. Kwetu pale Chalinze, madereva wa malori wanasimamisha magari makubwa kunywa pombe, viroba. Baada ya kulewa kabisa ndiyo wanaingia katika magari yao wakidai kuwa pombe inawaongezea ufanisi wa kuendesha malori. Upuuzi gani huu?”

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.