2015-06-19 08:23:00

Unganisheni: Udhaifu, Sala na Msamaha ili kuonja huruma ya Mungu!


Pamoja na kwamba tu dhaifu, ni lazima tuwe na uwezo wa kusamehe. Maneno matatu yaunganike pamoja: Udhaifu, Sala na Msamaha. Mkristo anaweza kusali vizuri endapo tu  anawenza kusamehe na kujijengea moyo wa amani.  Hayo ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri  yake aliyoyatoa Alhamisi, tarehe18 Juni 2015 katika Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko Mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amekaza kusema, Mkristo lazima afahamu kwamba, pasipo msaada wa Mwenyezi Mungu, hawezi kusonga mbele katika safari yake ya maisha. Baba Mtakatifu anasema, tu wadhaifu , udhaifu ambao sote twautwaa baada ya doa lile la dhambi ya asili. Yule anayedhani ana nguvu au ana uwezo wa kuushinda udhaifu peke yake bila msaada wa Mungu, anajidanganya, na mwishowe anabaki kuwa ni mtu anayegandamizwa na udhaifu mwingi anaoubeba ndani mwake.

Udhaifu huu unatufanya tuombe huruma ya Mungu  kwa sababu katika udhaifu wetu hatuwezi kufanya lolote bila ya msaada wake. Hatuwezi kupiga hatua katika maisha ya Kikristo pasipo msaada wa Mungu kwa sababu ya huu udhaifu wetu.  Wale waliosimama, wajiangalie wasije wakaanguka kwa sababu ni wadhaifu, na tena ni wadhaifu katika imani.

Baba Mtakatifu ameendelea kusema, sisi sote tunayo imani, lakini endapo hatutambui uhalisia wa udhaifu wetu, sote tutaishia kuangamia. Kwa sababu hiyo, sala hii ni nzuri isemayo “Ee Bwana, mimi ninatabua kwamba katika udhaifu wangu, siwezi kufanya lolote bila msaada wako”.

Akikazia juu ya wazo la sala, Baba Mtakatifu amesema, “Sala zetu hazihitaji kuwa na   wmengi sana”. Yesu ameonya “jifunzeni kusali” lakini “ si kama wapagani” ambao wanafikiri watasikilizwa kwa wingi wa maneno yao. Papa Francisko amemuelezea Mama ya Samueli ambaye alikuwa akimwomba Mwenyezi Mungu amjalie kupata mtoto, akawa akisali huku akibwabwaja mdomo.

Na kuhani aliyekuwapo pale, akidhani kwamba yule mwanamke alikuwa amelewa, alimkaripia kwa sababu midomo tu ilionekana kuchezacheza tu…hakuweza kutamka maneno, alikuwa anaomba mtoto.  Papa Francisko anasema husali hivyo mbele ya Mungu. Na katika sala tunatambua kwamba yeye ni mwema na anajua mambo yetu yote  na anajua mahitaji yetu; tuanze kwa kutamka line neno “Baba”, ambalo ni neno la kibinadamu, ambalo linaihuisha sala endapo tu tunalisema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu amekaza kusema, ‘tuanze sala kwa nguvu ya roho mtakatifu anayesali ndani mwetu’. Tusali hivyo kwa moyo mkunjufu  na katika uwepo wa Mungu ambaye ni Baba na anayejua mahitaji yetu hata kabla ya kuyatamka. Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko amekazia juu ya umuhimu wa msamaha kwa kusema “msamaha ni ngao kubwa, ni neema kutoka kwa Bwana”. Kama  vile Yesu alivyowafundisha wafuasi wake kwamba ‘kama wao hawasamehi makosa ya wengine, na vivyo hivyo Baba hatawasamehe makosa yao’.

Tunaweza tu kusali vizuri na kutamka ‘Baba’ kwa Mungu, endapo moyo wetu una amani na ndugu zetu. Hata kama umekosewa mambo mengi kiasi gani, wewe samehe. Samehe naye pia atakusamehe. Na hivyo udhaifu tulionao, kwa msaada wa Mungu unafanywa kuwa ngao kwa sababu msamaha ni ngao. Yahitaji kuwa wajasiri ili kuweza kusamehe, lakini ujasiri huu ni neema ambayo sisi tunahitaji kuipata kutoka kwa Mungu, kwa sababu sisi ni wadhaifu.

Na Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.