2015-06-19 08:56:00

Sanda Takatifu inagusa mateso na mahangaiko ya watu wengi duniani!


Kuna mamillioni ya watu ambao wamekuwa wakifanya hija ya kiroho, ili kutembelea na kutafakari mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanayojionesha kwenye Sanda Takatifu. Kunako mwaka 1973, Mwenyeheri Paulo VI, katika ujumbe wake wakati wa Onesho la kwanza alisikika akisema kwamba, pamoja na tafiti na hitimisho mbali mbali zitakazofanywa na wanasayansi kuhusiana na Sanda Takatifu, lakini hapa kuna sura ya Mungu kweli na Mtu kweli, inayoonesha mateso ya mwanadamu.

Kunako mwaka 1998, Mtakatifu Yohane Paulo II alitambua na kuthamini mchango uliokuwa umetolewa na wanasayansi kwa kutumia vipimo vya kisasa ili kutambua uhalisia wa Sanda Takatifu na kukiri kwamba, Sanda Takatifu ni changamoto kubwa kwa akili ya mwanadamu. Papa Yohane Paulo wa Pili aliwataka wanasayansi kuendelea na uchunguzi wao, lakini wakiheshimu imani ya waamini, kwani Sanda Takatifu inaweza kufananishwa kama kioo cha Injili.

Hii ni sura ya mwanadamu anayeendelea kuteseka, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Sanda Takatifu ni ishala ya ukimya unaowachangamotisha waamini kulitafakari kwa kina Fumbo la Msalaba wa Kristo na kwamba, kifo si hatima ya maisha ya mwanadamu, kwani baada ya kifo, kuna maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 alitembelea Jimbo kuu la Torino, ili kutoa heshima zake kwa Sanda Takatifu na hatimaye kusema kwamba, Sanda Takatifu ni kielelezo cha Jumamosi kuu, inayoonesha kimya kikuu na mwendelezo wa mchakato wa mbegu iliyozikwa ardhini, iweze kuchipua na kuzaa matunda ya matumaini. Sanda Takatifu inagusa giza la imani, lakini pia ni mwanga wa matumaini yasiyokuwa na mwisho.

Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013, mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alisema, Sanda Takatifu inaonesha macho yaliyofumbwa, na mwili wa maiti, lakini bado unaendelea kuwaangalia watu na katika ukimya wake, maiti hii, inazungumza na kuwahoji watu kutoka katika undani wa maisha yao. Hii ni sura inayoangalia kwa upendo na hakuna cha zaidi kinachotafutwa na sura hii.

Katika kitabu cha kumbu kumbu ya mahujaji waliotembelea na kusali mbele ya Sanda Takatifu, hakuna hata mtu mmoja aliyeomba kufanyiwa muujiza, maneno ya mshangao na shukrani ndiyo yanayoonekana kwa wingi. Sanda Takatifu inazungumza kuhusu Yesu Kristo, lakini kwa namna ya pekee, inagusa mateso na mahangaiko ya watu wengi wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wenye madonda makubwa katika maisha yao; watu ambao utu na heshima yao vimewekwa rehani kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso.

Sanda Takatifu inaonesha michirizi ya damu, kielelezo cha Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu ametwaa mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuwashirikisha upendo wa Mungu, ndivyo anavyoandika Roberto Gottardo, Rais wa Tume ya Sanda Takatifu, Jimbo kuu la Torino, wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko, Jimboni humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.