2015-06-19 15:28:00

Msijilimbikizie mali duniani, mtakumbwa na msongo wa mawazo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 19 Juni 2015 amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiwekea akiba mbinguni badala ya kumezwa na malimwengu kwa kutaka kujilimbikizia utajiri na mali, mambo ambayo kimsingi yamekuwa ni chanzo cha vita; kusambaratika kwa tunu msingi za maisha ya kiutu na kifamilia pamoja na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, utajiri unamtendea mtu katika maisha yake na wala si kama sanamu tu, kwani daima unamhamasisha mtu kuuongeza na matokeo yake unachukua nafasi katika maisha na moyo wa mwanadamu. Kama mtu hatakuwa makini, ataishia kuwa ni fisadi na mla rushwa, badala ya kuokoa moyo wake kwa kutumia utajiri kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Kristo Yesu, anawafundisha wanafunzi wake kutojiwekea hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba, bali wajiwekee hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu; wala wevi hawavunji wala hawaibi, kwa kuwa hazina yao ilipo, ndipo utakakokuwepo moyo wao.

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, dhana ya kutaka kujilimbikizia mali ni kutaka kuwa na usalama na uhakika wa maisha, lakini matokeo yake, ni mtu kuwa mtumwa wa mali na utajiri, kiasi hata cha kuharibu utu na heshima ya mtu. Uchu wa fedha na mali ni hatari kwa maisha ya binadamu, kwani mtu anadhani kwamba, akiwa na mali nyingi anakuwa na nguvu na usalama wa kiuchumi.

Kimsingi, binadamu anatabia ya kutaka kujikusanyia utajiri na mali, ili kutawala na kuutiisha ulimwengu, matokeo yake ni mapambano ya kila siku. Mali na utajiri wa dunia, vinapaswa kuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utajiri uwe ni chombo cha huduma ya upendo na mshikamano kati ya watu.

Watu waliokirimiwa utajiri wamedhaminishwa huduma hi ina Mwenyezi Mungu, wanapaswa kuutumia vyema na kamwe wasichezee moto wa utajiri, utawafikisha mahali pabaya. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wajitahidi kutafuta utajiri utakaowawezesha kwenda mbinguni, ili kufuarahia maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.