2015-06-19 16:00:00

Hamasisheni utume wa Bibilia, ili waamini wakutane na Kristo Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 19 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Biblia vya Kanisa Katoliki pamoja na kumshukuru Askofu mkuu Vincenzo Paglia aliyemaliza muda wake wa uongozi pamoja na kumkaribisha Kardinali Luis Antonio Tagle ambaye amechaguliwa hivi karibuni kuwa Rais mpya wa Shirikisho hili, Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi.

Baba Mtakatifu anasema, ili kuweza kuhubiri Neno la Mungu kwa ari na moyo mkuu, kuna haja kwanza kwa wahubiri wenyewe kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika maisha yao ya kila siku. Familia ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa linachangamotishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumfahamu Kristo Yesu, wanalisoma na kulitafakari Neno la Mungu; wanalitangaza na kulishuhudia; wanajifunza na kulieneza.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kanisa linaheshimu daima Maandiko Matakatifu na kuyatumia katika Liturujia ili kujilisha na kuwalisha waamini wake, ili liweze kuwafaidia, kwa kuwa egemeo na nguvu kwa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi katika Kanisa la Kristo. Wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Ufunuo, yaani “Dei Verbum” kuna haja ya kujikita katika tafakari ya kina kuhusu Waraka huu kwa kutambua kwamba, Neno la Mungu ni chombo cha Uinjilishaji.

Wahakikishe kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yanafanyiwa kazi kama ilivyokaziwa pia na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika kunako mwaka 2008, ili kuweza kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa Mataifa, kama utekelezaji wa agizo la Kristo la kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji, ili Neno la Mungu liweze kupenya katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna maeneo ambayo Neno la Mungu bado halijawafikia watu wengi au halijapokelewa kama Neno la uzima. Kuna maeneo mengine ambayo Neno la Mungu halipewi tena thamani linalostahili, hali inayopelekea kumong’onyoka na hatimaye, kudumaa kwa maisha ya Kikristo na ari kwa Makanisa ya Kimissionari. Hapa wakristo wote wanawajibika katika ujumla wao, ikiwa kama Neno la Mungu litapoteza ladha yake kati ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha pekee kwa maisha na utume wa Kanisa, kwa kuhamasisha Utume wa Biblia, ili waamini waweze kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, kwani “kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo”. Mihimili ya Uinjilishaji iwasaidie waamini kukutana na Yesu Kristo ili kuamsha imani na kuleta mabadiliko katika maisha, kumbe, Utume wa Biblia hauna budi kuvaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.