2015-06-19 08:36:00

Hakuna upendo mkuu kuliko huu: Mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake!


Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Torino kuanzia tarehe 21 hadi 22 Juni 2015 inaongozwa na kauli mbiu “hakuna upendo mkuu kuliko huu”. Hii ni hija ambayo itamwezesha kutoa heshima zake kwa Sanda takatifu pamoja na kushiriki kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco.

Baba Mtakatifu Francisko, ataianza siku ya pili ya hija yake Jimboni Torino, Jumatatu tarehe 22 Juni 2015 kwa kutembelea Hekalu la Waamini wa Valdese lililoko Torino na hapo atapokelewa na viongozi wakuu wa Kanisa hili. Baba Mtakatifu atatoa neno kwa waamini wa Kanisa hili pamoja na kusikiliza hotuba mbali mbali zitakazotolewa na viongozi wakuu wa Kanisa la Valdese. Hizi ni juhudi za kudumisha majadiliano ya kiekumene, ili kwa pamoja kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa amri ya Kristo, ili wote wawe wamoja.

Baba Mtakatifu Francisko atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na ndugu zake kwa faragha, kwani itakumbukwa kwamba, kwa asili Baba Mtakatifu Francisko anatoka kwenye mkoa wa Piemonte, ulioko Kaskazini mwa Italia. Ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili yao na baadaye, kupata chakula cha mchana kwa pamoja.

Kabla ya kuondoka Uaskofuni, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na wajumbe wa Kamati ya Sanda Takatifu na walioshiriki katika maandalizi ya hija yake ya kitume. Kutakuwa na umati wa vijana utakaokuwa umejipanga toka Uaskofuni hadi kwenye Uwanja wa ndege wa Torino. Baada ya kutua kwenye Uwanja wa ndege wa Ciampino, Baba Mtakatifu Francisko ataelekea moja kwa moja mjini Vatican.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino anasema kwamba, Sanda Takatifu inagusa undani wa imani ya Wakristo, kwani hiki ni kielelezo makini cha Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Mateso ya Yesu yanagusa shida na mahangaiko ya binadamu katika nyakati mbali mbali. Ni udhaifu na mapungufu ya binadamu kutokana na dhambi. Sanda takatifu si sehemu ya imani wala ushuhuda wa ufufuko wa Yesu Kristo bali ni hija ya maisha ya kiroho inayowahamasisha waamini kufanya toba na wongofu wa ndani ili kuambata matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia anakaza kusema kwamba, Sanda Takatifu ni kielelezo cha upendo mkuu unaobubujika kutoka kwa Yesu. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Torino. Huu ni upendo ambao Yesu ameuonesha kwa kujisadaka, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, tayari kumshirikisha maisha ya uzima wa milele. Hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha waamini kujikita katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jimbo kuu la Torino, limewaalika vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia kwenda Jimboni humo ili kusherehekea kwa pamoja, Jubilei ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, mtume wa vijana. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kujiachilia mikononi mwa Yesu ili aweze kuwaangalia, ili katika Sanda Takatifu ambayo ni kielelezo cha kifo, waweze kuona chemchemi ya Injili ya Maisha.

Sanda Takatifu si masalia matakatifu, lakini bado inaendelea kuwa fumbo kubwa kwa wanasayansi na katika historia. Mahujaji wanaoendelea kumiminika Jimboni Torino wanafanya hija ya imani inayoimarishwa kwa uzuri unaoambata imani na wala si miujiza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.