2015-06-16 15:09:00

Umaskini ni kiini cha Injili ya Kristo! Msiwabeze maskini!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 16 Juni 2015 anasema kwamba, umaskini ni kiini cha Injili kwani pasi na umaskini, ni vigumu sana kuelewa ujumbe wa Yesu Kristo kwa Watu wa Mataifa. Si haki kuwabeza viongozi wa Kanisa wanaosimama kidete kutetea utu na heshima ya maskini kwa kuwaita eti hao ni “Wakomunisti”.

Mtakatifu Paolo alikuwa mstari wa mbele kukusanya msaada kutoka kwenye Kanisa la Korintho ili kuwasaidia Wakristo waliokuwa wananyanyaswa na umaskini Yerusalemu na hapa ni mwanzo wa taalimungu ya umaskini katika maisha na utume wa Kanisa. Umaskini ni kiini cha Injili na kwamba, wakristo wanapaswa kuonesha utajiri wa maisha yao ya kiroho kwa kuambata: imani, Neno la Mungu, matendo ya huruma na upendo yanayoonesha imani inayomwilishwa katika matendo, kwa kutambua kwamba, ukarimu ni utambulisho wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Utajiri wa mali na vitu, ushuhudiwe pia kwa njia ya matendo ya huruma, kwani hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuongozwa na kanuni maadili inayoonesha ukinzani kati ya utajiri na umaskini. Imani ya kweli haina budi kushuhudiwa katika matendo, anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Kanisa la Yerusalemu lilikuwa maskini wa kiuchumi, lakini tajiri wa imani, kwani hapa ilikuwa ni hazina ya utajiri wa Maandiko Matakatifu. Kanisa la Korintho na Yersalemu yaliweza kubadilishana umaskini na utajiri, ambao ulitumika kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili waweze kutajirishwa na ukweli wa Injili katika maisha yao. Utajiri wa waamini usaidie mchakato wa Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Yesu Kristo aliyekuwa tajiri, lakini hakuona kwamba, ule utajiri wake ni jambo la kuambatana nalo sana, akaamua kuwa mtii na kujitwalia hali ya ubinadamu, katika mambo yote akawa sawa na binadamu, lakini hakutenda dhambi.

Hiki ni kielelezo cha Fumbo la Umwilisho na mwaliko wa kukumbatia Heri za Mlimani, ili kutajirishwa na Kristo, fukara, mtii na mseja. Ukarimu ni utambulisho na kielelezo cha Mkristo na kwamba, Wakristo wanahamasishwa kutajirishwa na umaskini wa maskini katika hija ya maisha yao, kwani maskini ni hazina na amana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukarimu wa kweli ni mchakato unaowatajirisha wale wanaotoa na wale wanaopokea kwa moyo wa shukrani.

Umaskini anasema Baba Mtakatifu Francisko si dhana ya kufikirika bali ni uhalisia wa maisha ya waamini, unaopata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka ya Kristo kwa binadamu. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kukita maisha yao katika ufukara wa Kiinjili kwa kutong’ang’ania na kumwezwa na malimwengu, bali kuwa na hekima ya kutumia vyema mambo ya dunia kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Yesu Kristo anaendelea kuonesha umaskini wake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Ibada ya Misa Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Yesu anawatajirisha waja wake katika  maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.