2015-06-16 16:09:00

Patriaki Moran Mor Ignatius Ephrem II kukutana na kusali na Papa Francisko


Kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 20 Juni 2015, Mheshimiwa sana Moran Mor Ignatius Aphrem wa pili, Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Siro la Antiokia na Mashariki yote, atakuwa na hija ya kichungaji mjini Roma na kilele cha hija hii ni kukutana na kusali kwa pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 19 Juni 2015. Patriaki Moran Mor Ignatius Aphrem wa pili alichaguliwa kunako mwaka 2014.

Kanisa la Kiorthodox la Siro ni Jumuiya ya Kikristo yenye makao makuu yake huko Antiokia, mji wenye historia na kumbukumbu kubwa ya maisha na utume wa Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Hapa ni mahali ambapo wamissionari wa kwanza walianza kutoka kifua mbele tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Hili ni Kanisa ambalo limeenea sana huko Syria, Uturuki, Iraq, Lebanon na Israeli.

Kutokana na uwepo wa wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, Wakristo kutoka Antiokia walijikuta wengi wao wakiwa wanaishi huko Marekani, Canada, Uingereza, Australia, New Zealand na India, ambako kuna idadi kubwa sana ya waamini wa Kanisa hili. Kuna uhusiano wa karibu sana na Kanisa Katoliki katika mambo mbali mbali. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 23 Juni 1984 Papa Yohane Paulo II na Patriaki Mor Zakka Iwas walitia sahihi tamko la pamoja kuhusu ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili na kuungama imani.

Kunako mwaka 1993 masuala ya ndoa mchanganyiko yalipewa ufumbuzi kwa kuzingatia Mkataba wa Kerala uliopitishwa na kuridhiwa na viongozi wa Makanisa haya mawili kunako mwaka 1994. Miongozo ya shughuli za kichungaji ilitolewa ili kuwasaidia waamini wa Makanisa haya kujenga na kuimarisha maisha ya ndoa na familia.

Patriaki pamoja na ujumbe wake wakati wa ziara yake ya kichungaji mjini Roma, atakutana pia na kuzungumza pamoja na viongozi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya uhamasishaji Umoja wa Wakristo na baadaye, atakwenda kusali kwenye kaburi la Mtakatifu Petro, lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.