2015-06-16 15:52:00

Kanisa ni chombo cha huduma kwa maskini na wahitaji!


Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa tangu kale, Kanisa la Mtakatifu Stefano Shahidi lililoko mjini Vatican, limekuwa ni mahali pa mahujaji waliokuwa wanafanya hija zao mjini Roma, ili kusali kwenye makaburi ya Wakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani pamoja na kuendelea kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo. Hii ni changamoto ya kuendelea kusikiliza kwa makini kilio cha mateso na mahangaiko ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia.

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa hili, yanalenga kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia waja wake  haki na amani huko Mashariki ya Kati hususan: Iraq na Syria ambako Wakristo wanaendelea kuteswa, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni muda wa kusali kwa ajili ya kuomba neema na nguvu ya uponyaji nchini Ukraine, bila ya kuwasahau wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kubisha hodi kwenje mipaka ya Nchi za Jumuiya ya Ulaya, ili kupata hifadhi ya maisha. Wengi wa wakimbizi na wahamiaji hawa ni wale wanaokimbia vita, machafuko ya kijamii na hali ngumu ya maisha huko Syria, Ethiopia na Eritrea.

Hivi ndivyo Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, alivyopembua wakati wa mahubiri yake kwenye Kanisa la Mtakatifu Stefano mjini Vatican, kwa ajili ya wajumbe wa Mkutano mkuu wa themanini na nane wa Shirika la Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO. Jumanne tarehe 16 Juni 2015 ni siku maalum iliyotengwa kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati, Ukraine na Eritrea.

Kardinali Sandri amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano wa upendo na udugu unaojionesha kwa njia ya huduma makini, kama ilivyojitokeza kwenye Kanisa la mwanzo. Lengo lilikuwa ni kudumisha amani pamoja na kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiini cha upendo unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa ni kielelezo cha umwilisho na udumisho wa upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Msaada unaotolewa kwa Wakristo waliokuwa wanateseka, ulipania kujenga utamaduni wa kuhudumiana kama ndugu katika Kristo, kama kielelezo makini cha mchakato wa Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Huduma ya upendo inaliwezesha Kanisa kutekeleza sera na mikakati yake katika shughuli za kichungaji kwa ujenzi wa: Makanisa mapya, shule, zahanati na nyumba za watoto yatima.

Hiki ni kielelezo cha Jumuiya inayojali na kuguswa na mahangaiko ya jirani zake bila ubaguzi wa aina yoyote ile, kwani Kanisa linatambua kwamba, binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huduma pasi na ubaguzi, ni mwendelezo wa maadhimisho ya Pentekoste mpya ndani ya Kanisa, kwa kutangaza kwa ari na moyo mkuu kwamba, Yesu aliteswa, akafa na kufufuka, kiini cha Habari Njema ya upendo na mshikamano kati yaWatu.

Kardinali Sandri anasema kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya zawadi na ukarimu unaojionesha ndani ya Kanisa, kwani kwa njia ya Yesu Kristo aliyekuwa tajiri, lakini kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, alijinyenyekesha, akawa maskini, ili katika umaskini wake, watu waweze kuonja utajiri wa Mungu. Huduma ya upendo ni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kristo na sehemu ya mchakato wa hija inayowapeleka katika ukamilifu wa maisha na huruma kama alivyo Baba yao wa mbinguni

Kardinali Leonardo Sandri amekamilisha mahubiri yake kwa kuwaweka waamini wote chini ya usimamizi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa upendo na huduma, aliyejisadaka kwa ajili ya kumhudumia binamu yake Elizabeth aliposikia kwamba alikuwa ni mjamzito. Bikira Maria ni mfano wa upendo na mshikamano wa kweli katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.