2015-06-15 08:53:00

Lindeni na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 14 Juni 2015 amezungumzia kuhusu ufanisi wa Neno la Mungu, umuhimu wa Ufalme wa Mungu, kiini cha matumaini na dhamana ya waamini katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu katika historia. Mbegu kadiri ya Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu lenye nguvu ndani yake inayoweza kulifanya kukua katika moyo wa mwamini anayelisikiliza kwa unyenyekevu kadiri ya mazingira yake ya kibinadamu.

Mwenyezi Mungu amemdhaminisha kila mwanadamu Neno lake na kwamba, ataliwezesha kukua na kuzaa matunda mengi. Ukuaji na ustawi wa Ufalme wa Mungu ni kazi inayofanywa na Mungu mwenyewe kwa kumshirikisha mwanadamu, ndiyo maana waamini wanamwomba Mungu ili Ufalme wake ufike hapa duniani. Katika mchakato huu, binadamu anashiriki, anatafakari na kufurahia kazi inayofanywa na Mwenyezi Mungu na kusubiri kwa uvumilivu matunda.

Neno la Mungu linasaidia kukuza maisha, mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi katika hija ya maisha yao, kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, ili kukuza na kustawisha Ufalme wa Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Katika mwono na mawazo ya kibinadamu, Ufalme wa Mungu unaweza kuonekana kuwa ni mdogo kuliko hata ile mbegu ya haradali, lakini una uwezo wa kukua na kuongezeka sana lakini unahitaji maskini wa roho, wanaotegemea nguvu ya upendo wa Mungu na kutenda kadiri inavyompendeza Mungu na wala si kwa ajili ya kuwafurahisha wanadamu.

Kwa njia hii anasema Baba Mtakatifu Francisko, nguvu ya Yesu Kristo inaweza kuleta mabadiliko katika maisha ya watu na matokeo yake kuonekana duniani na katika historia ya mwanadamu. Ili Ufalme wa Mungu uweze kukua na kuongezeka unahitaji ushirikiano mkamilifu wa binadamu, lakini kwa kutambua kwamba, hii ni kazi na zawadi ya Mwenyezi Mungu. Jitihada za mwanadamu ni kidogo sana, ikilinganishwa na matatizo pamoja na changamoto zilizoko duniani.

Lakini, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu haogopi matatizo, kwani anafahamu kwamba, ushindi utapatikana na upendo wake utawezesha mbegu njema kuzaa matunda kwenye uso wa dunia. Hii ndiyo imani na matumaini ya Kanisa, licha ya matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Mbegu ya wema na amani itakuwa na kukomaa, na watu wataonja upendo wenye huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni matumaini yasiyodanganya kamwe.!

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu aliwakumbusha mahujaji na waamini kwamba, Jumapili, ili kuwa ni Siku ya Kimataifa ya kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu walioko hatarini. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watu wote wanaochangia damu pamoja na kuwahimiza vijana wa kizazi kipya kuiga mfano bora wa watu kama hawa. Baba Mtakatifu pia ameungana na wale wote ambao wanaendelea kuwatafuta ndugu zao waliopotea katika mazingira ya kutatanisha pamoja na wanafanyakazi wanaotetea haki yao kama kielelezo cha utu wao.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea ufanisi katika uzinduzi wa Waraka wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, tukio litakalofanyika hapo Alhamisi, tarehe 18 Juni 2015. Tukio hili liwe ni fursa makini ya kulinda na kutunza mazingira kila mtu katika eneo lake. Waraka huu ni kwa ajili ya wote, kwani ni ujumbe unaohamasisha uwajibikaji wa nyumba ya wote ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.