2015-06-14 14:59:00

Tafakari ya Papa Francisko kwa Wakleri wakati wa mafungo ya kiroho Roma!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kwa Wakleri waliokuwa wanahudhuria mafungo ya kimataifa yaliyoandaliwa na Chama cha Uamsho wa Kikristo kwa kushirikiana na Chama cha udugu wa Kikatoliki amekazia umuhimu wa mshikamano wa kikuhani, wito na maisha ya kipadre kama jibu muafaka la upendo wa Kristo; umuhimu wa mahubiri kama sehemu ya mchakao wa kuwafunda waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kashfa ya utengano ambayo bado inalitendea Kanisa la Kristo.

Baba Mtakatifu Franciko, Ijumaa jioni tarehe 12 Juni 2015, wakati wa tafakari yake kwa wakleri amewapongeza kwa moyo wa upendo, mshikamano na umoja wa kidugu unaojionesha katika maisha na utume wa kikuhani kwa kwa wakleri wote kuwa pamoja katika kusali, kutafakari na kujadiliana uzuri na changamoto mbali mbali za maisha na utume wa kipadre. Lengo ni kusaidiana na kuimarishana katika maisha na utume wa Kipadre, kwa kuzingatia: ukweli, uwazi na upendo wa kidugu.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya namna hii inaweza kujengwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kumbe ni wajibu wa Wakleri kuomba neema na baraka za Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia nguvu ya kujenga Jumuiya kama hii, kwa kuwawezesha viongozi wa Kanisa kuwa karibu zaidi na waamini wao, ili kuwajenga na kuwaimarisha katika hija ya maisha yao ya Kikristo hapa duniani. Wakleri wajenge utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa, kwani pasipo na majadiliano, Kanisa litadumaa na hatimaye kupotea! Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Kanisa litaendelea kujengwa katika unafiki, sumu ya maendeleo ya kweli.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanawake wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa hata kama si Wakleri. Watambue kwamba, wao ni mfano wa Umama wa Kanisa na kielelezo cha Bikira Maria aliyekuwepo siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakajazwa nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa Watu wa Mataifa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwamba, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku maalum ya kuombea utakatifu wa Mapadre na kwa namna ya pekee wakati huu Mama Kanisa anapojikita katika Uinjilishaji wa kina unaohitaji kwa namna ya pekee ushuhuda wenye mvuto na mashiko, anawaalika wakleri kukita maisha yao katika mchakato wa utakatifu wa maisha kwa kutambua kwamba, upadre ni wito wa upendo unaojibiwa kwa upendo endelevu pasi na kukata tamaa!

Baba Mtakatifu anawataka wakleri pale wanapokumbana na vishawishi, wanapoanguka dhambini, wanapoelemewa na magonjwa pamoja na upweke, wasisite kukimbilia katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, hapo wataweza kujichotea tena nguvu ya kusonga mbele kwa ujasiri mkuu. Wakleri watambue kwamba, wao kweli ni marafiki wa Yesu na kamwe si watumwa wala wafanyakazi, bali wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Unafiki ni sumu mbaya katika maisha ya Wakleri kwani unawafanya kuwa na maisha ya ndumilakuwili, kumbe wanapaswa kuonesha wema na upendo kwa Watu wa Mungu, kwani watu wana kiu ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Uinjilishaji mpya ni mchakato unaotambua upendo endelevu wa Yesu katika maisha ya waja wake, changamoto na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda waaminifu wa upendo wa Kristo. Wakleri wasaidiane na kutaabikiana wakati wa shida na raha, kama inavyokuwa kwa wanandoa ambao wanaweza kudumu katika maisha na wito wao hata wakawa tayari kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya ndoa. Hapa kuna haja ya kuonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa kumwachia nafasi Yesu Kristo ili aweze kuwashirikisha upendo wake usiokuwa na mipaka wala mawaa!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakleri kujenga utamaduni wa kuhitimisha siku kwa kukutana na na kusalimiana na Yesu, walau hata kwa dakika chache kabla ya kwenda kulala na wala si kuhitimisha siku kwa kuangalia sinema kwenye luninga! Mapadre waandae vyema mahubiri yao kwa kutambua kwamba, mahubiri ni kisakramenti kinachowapatia waamini neema katika safari ya maisha yao ya kiroho.

Mahubiri yaguse undani wa maisha ya watu, kwani huu ni muhtasari wa Neno la Mungu na wala si somo la maadili. Mahubiri yasipoandaliwa vyema yanakuwa ni kero na waamini watautumia muda huu kwenda nje kuvuta sigara na kupigiana michapo ya maisha! Mahubiri yawe ni muhtsari wa ushuhuda wa maisha yanayomwambata Kristo.

Baba Mtakatifu anawataka wakleri wahakikishe kwamba, wanawapatia watu Sakramenti za Kanisa na kamwe wasiwanyime wazazi kubatiza watoto wao kutokana na mapungufu yao ya maisha kwani Sakramenti ya Ubatizo ni mlango wa neema ya wokovu. Mapadre wajitahidi kuonesha wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Wawe tayari kuwapatia waamini Sakramenti ya Upatanisho, kwa kuwasikiliza kwa umakini na kuwapatia ushauri katika safari ya maisha yao, tayari kurudi tena kujipatanisha na Mungu wanapoanguka dhambini. Waamini wajengewe hamu na ari ya kupenda kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utengano miongoni mwa Wakristo ni kashfa ambayo bado inaendelea. Hapa wakristo hawana budi kujielekeza zaidi katika majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika Uekemene wa maisha ya kiroho na kimaadili, ili kwa pamoja waweze kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wakristo wajitahidi kuganga madonda ya chuki na uhasama, kwa kukazia upendo na uekemune wa damu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza kwa namna ya pekee wanachama wa Uamsho wa Kikatoliki kwa kuwasaidia watu kukutana na Kristo anayewakarimia neema ya kuanza upya maisha yao, tayari kuambatana na Yesu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mguso! Anawataka waamini walei kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu amewapatia wakleri waliokuwa wanahudhuria mafungo ya maisha ya kiroho kimataifa hapa mjini Roma zawadi ya Nyaraka zake kuhusu: Injili ya Furaha, Evengelii gaudium na Uso wa huruma, Misericordiae vultus.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.