2015-06-14 14:41:00

Jitahidini kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Kwa mara nyingine tena karibu katika kipindi hiki tuendelee kuuelewa waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; kama kawaida jina lake ni Misericordiae vultus, yaani uso wa huruma.

Lengo letu: kwa tafakari ya Waraka huu tunataka tuelewe vema umaana na uzito wa huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu, na hivyo tutakapo adhimisha Mwaka Mtakatifu wa  Jubilei yetu tusiwe wageni. Jubilei hiyo itazinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8.12.2015 na kuhitimishwa rasmi Katika sherehe ya Kristo Mfalme Mwezi Novemba 2016.

Katika kipindi kilichopita, Baba Mtakatifu ndani ya Misericordiae vultus alilialika Kanisa kurudi kwenye misingi. Moja ya tabia ya msingi ya Kanisa ni “huruma”. Ni kwa njia tu ya huruma inayomwilishika, Kanisa linaweza kutekeleza vema wajibu wake msingi wa kuwa Sakramenti ya Jumla ya Ukombozi wa wanadamu. Ni kwa njia ya huruma pekee Kanisa linaweza kutekeleza vema wajibu wake wa kimisionari, wa kuwaendea watu wote ambao bado hawajaisikia sauti ya Injili na kuwahubiria ili wapate kuamini, kubatizwa na kuokoka.

Na tena kwa njia ya huruma hiyo hiyo Kanisa litaweza kuwaendea watu waliogalagazwa na ibilisi katika vumbi la dhambi, na kuviringishwa kwenye ukurutu wa umasikini na ugumu wa maisha, ili kuwahubiria injili ya furaha matumaini na uwajibikaji. Kwa njia ya huruma hiyo hiyo Kanisa litaweza kutoka kuwaendea watu wote wanaoogeshana damu za vita, wanaonusishwa harufu ya vifo kila siku, hawana uhakika wa kuwa hai takika chache zijazo;  wanaosikilizishwa milindimo ya mitutu na mabomu kila kukicha, na kuwahubiria,Injili ya msamaha, amani na mapatano ya kweli na ya kudumu. Huko ndiko kutwaa madhaifu na mahangaijo ya kaka na dada zetu.  Kwa mwangwi wa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko, huruma haswa – ni kitenda kazi cha Mama Kanisa. Ni kwa sababu hiyo, amelialika Kanisa kuivaa huruma kwa moyo wote.

Leo ndani ya Misericordiae vultus,  yaani Uso wa huruma, Baba Mtakatifu Francisko anatualika, tusiusahau utajiri uliofumbatwa katika Barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II, ijulikanayo kwa jina la Dives in misericordia; maana yake utajiri katika huruma, ambayo  wakati ilipotolewa bila kutegemewa, iliwashangaza wengi. Kuna vipengele viwili ambavyo ningependa kuviwekea mkazo, anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Kwanza kabisa Mtakatifu Yohane Paulo wa II, aliuangazia ukweli kwamba tumesahau tema ya huruma katika utamaduni wa leo. Alisema “fikra za siku zetu hizi, zaidi ya zile za watu wa zamani, zinaelekea kupingana kabisa na Mungu wa huruma, na kwa hakika zinaelekea kumtenga na maisha huyo Mungu wa huruma, na kufuta kabisa wazo la huruma mioyoni mwao. Neno na dhana ya huruma linaelekea kumtaharukisha mwanadamu ambaye kwa msaada wa maendeleo ya sayansi na teknolojia amekuwa mdau wa ulimwengu, ameutiisha na kuumiliki (Rej.Mwa. 1:28).

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumnukuu  Mtakatifu Yohane Paulo wa II, ndani ya Dives in Misericordia aliyesema, Huku kuutawala ulimwengu, wakati mwingine kumeeleweka kwa upande mmoja na katika maana ya juu juu tu; inaelekea kutokuwa na nafasi kabisa kwa ajili ya  huruma , na ndiyo maana katika hali halisi ya Kanisa na ulimwengu katika siku zetu hizi, watu wengi na makundi ya watu wakiongozwa na hali ya imani hai wanairudia huruma ya Mungu.

Zaidi ya hayo, Mtakatifu Yohane Paulo wa II alihimiza sana juu ya utangazaji na ushuhuda wa huruma katika ulimwengu mambo leo. Hilo linajikita katika upendo kwa mwanadamu, kwa sababu nyakati hizi  chochote kilicho cha kibinadamu kinazingirwa na hatari kubwa kadiri ya mifumo ya walimwengu wa nyakati zetu. Mtakatifu Yohane Paulo wa pili ndani ya Dives in misericordia, mintarafu utangazaji wa huruma alikaza kusema; “Fumbo la Kristo linanilazimu mimi kutangaza huruma kama huruma ya upendo wa Mungu, inayofumbuliwa katika fumbo lilelile la Kristo”.

Kwa namna hiyo hiyo Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, nami pia “inanilazimu kuikimbilia huruma hiyo na kuiomba katika wakati huu mgumu wa historia ya Kanisa na ulimwengu”. Fundisho hili ni mwafaka zaidi na linastahili kuzingatiwa kwa namna ya pekee katika Mwaka huo Mtakatifu wa Huruma ya Mungu.

Anaendelea kusema “Tuyasikilize kwa mara ngingine maneno haya: Kanisa linaishi maisha halisi wakati tu linapoungama na kutangaza huruma”. Hiyo ndiyo ndiyo sifa ya Mungu Baba na ya Mwana Mkombozi. Kanisa pia linaishi uhalisia wake linapowaleta watu karibu zaidi kwa Kristo aliye asili ya huruma, ambayo Kanisa lenyewe limedhaminishwa kuigawa.Tukingalimo mwezi Juni tunapouheshimu moyo Mtakatifu wa Yesu, Moyo wa Huruma, Moyo wa Mapendo, tuendelee kusali tukisema: Ee Yesu mwenye moyo Mpole na mnyenyekevu, ufalme wako ufike, utujalie mapendo yako na amani maishani ni mwetu;  na ufanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.

Mpendwa msikilizaji asante kwa kuitegea sikio Radio Vatican, kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.