2015-06-13 14:28:00

Skauti wafunika mjini Vatican, yaani imebaki kuwa ni gumzo la Jiji!


Wanachama wa Skauti kutoka sehemu mbali mbali za Italia, Jumamosi, tarehe 13 Juni 2015 tangu alfajiri na mapema, walianza kuupamba mji wa Roma kwa nyimbo na  matembezi ya ukakamavu kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wa zamani na vijana wa kizazi kipya walionekana kuwa na nyuso za furaha, licha ya safari ndefu waliyoifanya kutoka katika maeneo yao, vijana hawa wanasema, inalipa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewahakikishia wanachama wa Skauti kwamba wao ni amana kubwa ya Kanisa nchini Italia, pengine kwa wanachama wadogo hawawezi kulitambua jambo hili kwa haraka, lakini kwa vijana wa zamani, wamekuwa ni msaada mkubwa katika malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia kwa kuwasaidia wazazi na walezi katika utekelezaji wa dhamana ya malezi kwa watoto na vijana. Wazazi wanawaamini walezi wa Skauti kwa sababu wanatambua wema na hekima ya malezi ya Kiskauti yanayojikita katika tunu msingi za maisha ya binadamu; mazingira, maisha ya kiroho na imani kwa Mwenyezi Mungu.

Hizi ni mbinu zinazowafunda Maskauti kuwa kweli huru na kuwajibika barabara katika matendo yao; imani hii ya wazazi inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote, bila kulisahau Kanisa na kwamba, daima wanapaswa kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Jumuiya kubwa ya Kikristo. Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, mwaka jana wakati walipokuwa wanafanya matembezi ya kitaifa aliwapigia simu kwa kuwaambia kwamba, wanaongozwa na “Katiba ya Ujasiri”, kielelezo cha mambo msingi wanayokumbatia na matarajio yaliyomo mioyoni mwao. Haya ni masuala ya elimu, usikivu makini unaopaswa kuoneshwa na viongozi wao bila kusahau mchango wa Parokia na Kanisa katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Muasisi wa Chama cha Skauti Bwana Baden Powell anakiri kwamba, dini ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya wanachama wa Skauti kwani ni sehemu ya maisha yao, kwa kutambua uwepo wa Mungu na huduma. Hiki ni chama ambacho kinaendelea kuwekeza zaidi katika masuala ya maisha ya kiroho kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanachama wake wanapewa malezi ya imani; mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga, kwa ajili ya mafao ya wanachama wa Skauti.

Baba Mtakatifu anawapongeza wanachama wa Skauti kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; mchakato ambao unapaswa kuwa ni endelevu kama sehemu ya malezi na majiundo makini ya vijana, ili waweze kuimwilisha Injili inayowaletea mabadiliko katika maisha.

Baba Mtakatifu anasema kwamba vyama vya kitume ndani ya Kanisa Katoliki vina nafasi ya pekee kabisa katika maisha yake kwani huu ni utajiri wa Kanisa ambao ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji katika medani mbali mbali za maisha. Chama cha Skauti nchini Italia, kinaweza kuwa ni chachu ya Uinjilishaji kwa kudumisha madaraja ya majadiliano na jamii. Dhamana hii inaweza kutekelezeka ikiwa kama Skauti itaendelea kushikamana na Parokia zao pamoja na kushiriki kikamilifu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Kanisa mahalia, kwa kushirikiana kikamilifu na viongozi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali.

Baba Mtakatifu anawataka Skauti wasikubali kuwa ni mapambo wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu Jumapili au kwenye Sherehe kubwa. Anawapongeza Maskauti wote wanaoshirikiana na kushikamana na wenzao katika shughuli mbali mbali, kwani mambo yote haya ni utajiri mkubwa katika majiundo yao. Kwa hakika, uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ulipambwa na Skauti kutoka sehemu mbali mbali za Italia, uwepo wao umetikisa na kufunika mji wa Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.