2015-06-13 08:27:00

Kitimtim cha uchaguzi mkuu nchini Tanzania; Pinda atangaza nia!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amechukua fomu za kuomba kuwania Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Waziri Mkuu Pinda alikabidhiwa fomu hizo Ijumaa, Juni 12, 2015), saa 4:03 asubuhi kutoka kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Oganaizesheni), Bw. Mohammed Seif Khatib na saa 4:05 akaweka saini kwenye daftari la kupokea nyaraka ili kuthibitisha kuwa amezipokea.

Saa 4:07 alikabidhiwa mkoba wenye nyaraka hizo na Bw. Khatibu na saa 4:08 akaunyanyua juu mbele ya waandishi wa Habari waliokuwepo kwenye ukumbi wa Katibu Mkuu wa CCM kushuhudia akipokea fomu hizo. Kisha saa 4:15 aliingia ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kukutana na wanahabari.

Akizungumza na waandishi wa habari na wanaCCM waliofika ukumbi wa NEC kumsikiliza mara baada ya kuchukua fomu hizo, Waziri Mkuu alisema endapo atafanikiwa kuteuliwa na CCM awanie kiti cha Urais atasimamia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Uchumi ili unufaishe makundi mengi zaidi ya jamii.

“Ukuaji wa uchumi uko vizuri lakini umaskini unapungua kwa kiasi kidogo, kasi yake hairidhishi… hii ni kwa sababu ukuaji huo umegusa sekta zisizogusa maisha ya watu moja kwa moja kama za ujenzi, utalii, uchukuzi na nyinginezo,” alisema.

“Wataalamu wa mataifa yaliyoendelea wanatuambia ukuaji wa uchumi hauonekani sana kwa sababu unagusa maisha ya watu wachache, sasa hivi wanataka jitihada ziongezwe kwenye jamii kubwa zaidi ambazo ni wakulima, wavuvi, wafugaji, wajasiriamali na warinaasali,” alisema.

“Mimi naamini tukiwagusa hawa impact kubwa itaonekana, ajira zitapatikana kwani viwanda vya usindikaji vitakuwepo; kilimo kikiboreshwa kwa kutumia zana za kisasa wengi watafanya kazi hiyo ambayo hivi sasa kila mtu anaikimbia kwa sababu ya shuruba za kazi yenyewe.”

Alisema Mpango wa Kwanza wa Maendeleo na Ukuzaji Uchumi ulilenga kuimarisha miundombinu zikiwemo barabara, bandari na ndani yake kulikuwa na mpango wa kuunganisha makao makuu ya mikoa yote kwa barabara za lami ifikapo mwaka 2018.

Alisema mpango huo ulioasisiwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ni wa miaka 25 (2000-2025) lakini ilibidi Rais Kikwete augawanye katika awamu tatu za miaka mitano mitano kuanzia kwama 2011 -2015 sababu muda uliobakia ulikuwa ni miaka 15 tu.

“Kwa maoni yangu kazi iliyokwisha kufanyika ni nzuri lakini tusibweteke. Chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Uchumi, mambo yatabadilika na ikiwezekana hatutafika 2025 kwa sababu maji, elimu, afya vitakuwa vimeboreshwa tayari,” aliongeza.

Akigusia kuhusu Ilani ya CCM, Waziri Mkuu alisema hawezi kuiongelea kwa sababu bado haijatoka. “Lakini ninaahidi, pindi ikitoka na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM, na Mungu akijalia nikapitishwa na chama, sitashindwa kuitekeleza Ilani hiyo. Nina uzoefu wa Ilani zote zilizopita,”alisisitiza.

Alisema kufanya kazi kwa karibu zaidi na Marais wote wanne na uwepo wake kwenye Serikali za Mitaa kwa muda mrefu ni turufu pekee anayoamini itamuwezesha kuwahudumia Watanzania vizuri zaidi kwani anaifahamu nchi kwa undani pamoja na matatizo yanayowakabili Watanzania walio wengi.

Alisema anaamini Mungu peke yake ndiye ajuaye nani amemuandaa kwa ajili ya kuiongoza nchi hii na kwamba hata yeye bado anamtumaini Mungu amuongoze katika safari hiyo. “Mungu peke yake ndiye anajua nani amemuandaa kwa nafasi hii, ni siri yake. Kadri itakavyompendeza, atampa nafasi hiyo yeye amtakaye,” alisema.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.